Cosmus Hinzano ,31, kutoka Malindi alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Celestine Mahenzo ,26, ambaye alimuacha hivi majuzi.
Cosmus alisema mkewe aligura ndoa yao ya miaka 10 baada ya kugombana kwa nyumba wakati alipotoroka malazi yao.
Aidha, alidai kuwa mkewe haeleweki kwani kila wakati wakikosana ajaribu kumuuliza shida ni nini huwa anakimbia kuambia wengine.
"Hiyo siku ambayo tulikosana, alikuwa amehama chumba chetu cha kulala. Hiyo wiki ilikuwa ya makambi, akahama kitanda changu akaenda kwa watoto. Mimi sikutaka watoto waelewe vibaya. Nilimuita na kumuuliza shida ni nini. Hakutaka kunieleza, alikuwa anaambia watu wengine," Cosmus alieleza.
Cosmus alisema bado hajachukua hatua ya kumfuata mkewe kwani amewahi kuenda kwao mara nyingi hadi amechoka.
"Nimechoka, nilikuwa napumua niende tena. Nitaenda lakini napumzika ili kwanza nipate nafuu. Simuelewi," alisema.
Celestine alipopigiwa simu aliweka wazi kuwa tayari amemtema baba huyo wa watoto wake wanne na kumtaka asimfuate.
Aidha, aliomba kupewa muda wa miaka miwili kabla ya kufanya uamuzi wa ikiwa atarudi ama hatarudi.
"Bado hajafika nyumbani.Mimi niko nyumbani. Asije kabisa nilitoka mimi. Kila mmoja afuate shughuli zake Napumzika kabisa. Alisema sina adabu. Atafute bibi mwingine mwenye adabu aoe waishi kwa amani," alisema.
Aliongeza, "Watoto baki nao mwenyewe.Tafuta mwenye adabu uoe, mimi nifanye shughuli zangu.. Labda anipatie muda wa miaka miwili niangalie kama nitarudi ama sitarudi."
Cosmus alijaribu kumbembeleza mkewe aeleze kama kuna shida nyingine huku akimkumbusha kuhusu mtoto wao mchanga ambaye aliacha nyuma.
"Kuna mtoto ambaye siwezi kumlea saa hii anahitaji mama yake. Ni shida gani ulipitia hadi kusema hutaki tena kwangu," alisema.
Celestine alifichua kuwa kabla ya kutoroka, Cosmus alimshambulia na kumpa vitisho mbaya mbaya.
"Alinipiga sana akisema ananitia adabu. Alisema atanikata shingo, sasa mtu akinikata shingo nitakuwa hai kweli," alisema.
Cosmus alijitetea kwa kusema, "Nilikuwa na hasira sana. Nilijaribu kumbembeleza karibu masaa nne aseme shida ni nini, hakutaka kusema. Nilimtoa kwa chumba cha watoto akaenda nje. Niliona akikaa nje aumwe na nyoka, nani atamuulizia? Nilipomrudisha kwa nyumba, Alibomoa ili apite nje hasira ikanipanda nikampiga."
Celestine alipoombwa ashushe roho chini alisisitiza kuwa anahitaji muda wa miaka miwili kabla ya kufanya uamuzi.
Cosmus alisema, "Hakuna shida. Vile ameamua ni maiak miwili, siwezi kusubiri miaka miwili. Yeye kama anaweza kuvumilia miaka miwili, kama atamaliza miaka miwili kwao asahau kabisa."
Aliendelea, "Celestine ukifuata ya watu utasumbuka akili sana. Changamoto katika maisha ni shida. Mimi ruhusa ya kukupa miaka miwili sina. Nitakuja niongee na wazazi wako. Vile wataniambia ni hivo. Nakupenda sana. Nilikutoa kwen. Kama kuna mtu anakusumbua akusumbue kabisa."
Celestine alisema hana maneno ya kumuambia Cosmus.
Je, ushauri wako ni upi?