Patanisho: "Hata kama ameolewa na ako mimba, mimi nitamchukua hivo!" -Patrick

Margaret alithibitisha kuwa tayari yupo kwenye ndoa nyingine na hata kuna mipango ya harusi.

Muhtasari

•Bw Okumu alisema mke wake aligura ndoa yao ya miaka nane baada ya kuchoshwa na tabia zake mbaya.

•Margaret alisema Okumu anafahamu fika kuwa yupo kwenye ndoa nyingine na hata anamjua mumewe mpya.

Patrick Okumu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Margaret Nasambu ambaye alitengana naye mwaka jana.

Bw Okumu, dereva wa masafa marefu, alisema mke wake aligura ndoa yao ya miaka nane baada ya kuchoshwa na tabia zake mbaya.

"Mimi na mke wangu tulipendana tangu tupatane. Alikuwa amekubali kuolewa na kushi na mimi. Tulipooana tabia zangu zikawa hazimfurahishi. Kila mara nikimuona akitumia simu nilikuwa naudhika na kumgombanisha," alisema.

Okumu alikiri kwamba aliwahi kuvunja simu mbili za mkewe kutokana na wivu.

"Alikaa na mimi kwa ndoa akanivumilia hadi msimu wa Corona.Shetani aliniingia nikamfukuza mke wangu. Baada ya kumfukuza nikaanza kujuta. Baadae alisema tayari ashamove on na hawezi kurudi," alisema.

"Mimi bado nampenda sana. Sijui kama ni kweli lakini nasikia kuwa ameoleka na ana mimba. Ata kama ako na mimba na ameolewa mimi nitamkubali hivo, najua mimi ndio mwenye makosa," alisema Okumu.

Margaret alipopigiwa simu alithibitisha kuwa tayari yupo kwenye ndoa nyingine na hata kuna mipango ya harusi. Pia alifichua kuwa ni mjamzito na kutupilia mbali uwezekano wa kurudiana na Bw Okumu.

"Haiwezekani kurudiana kwa sababu mimi tayari nimeolewa. Labda tu asaidie mtoto wake. Nina bwana, ata tunapanga harusi Desemba. Niko na ujauzito wa miezi minne," alisema.

Margaret alibainisha kuwa Okumu anafahamu fika kuwa yupo kwenye ndoa nyingine na hata anamjua mumewe mpya.

Aidha alithibitisha kuwa mumewe huyo wa zamani amekuwa akilipa karo ya mtoto wao na kumuomba aendelee.

Baada ya kuona hakuna uwezekano wa kurudiana na aliyekuwa mkewe, Okumu alisema, "Basi aniambie maneno mazuri tu kwa sababu niko barabarani nisije nikapata ajali. Tayari nimeanza kupatwa na kizunguzungu."

Margaret hata hivyo alisisitiza hawezi kurudiana na Okumu na kueleza kuwa hata wazazi wake walimshauri dhidi ya kufanya hivyo.

"Mambo ya kupendwa nishapendwa na huyu mwingine. Muonyeni dhidi ya kutuma meseji za matusi kwa bwanangu,"