Patanisho: Jamaa alalamika vikali mkewe kumnyima chakula kwa mwaka moja

"Nilikuwa natoka kazi, hashughuliki na mimi ata kama nimechoka. Asubuhi hashughuliki na mimi," alilalamika.

Muhtasari

•Nyongesa alisema ndoa yake ya miaka 12 ilisambaratika baada ya mkewe kutomshughulikia kwa takriba mwaka mmoja.

•"Aliniweka kidole kwa macho. Nikamwambia ni heri atoke ama nitoke. Akaenda kwao. Alibeba mtoto wa mwaka mmoja,"alisema.

Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Jamaa ambaye alijitambulisha kama Ibrahim Nyongesa ,32, kutoka kaunti ya Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Josylynn ,27, ambaye alikosana naye takriban miezi miwili iliyopita.

Nyongesa alisema ndoa yake ya miaka 12 ilisambaratika baada ya mkewe kutomshughulikia kwa takriba mwaka mmoja.

"Ilikuwa ni mambo ya kisirani ya boma. Nilikuwa natoka kazi, hashughuliki na mimi ata kama nimechoka. Asubuhi hashughuliki na wewe. Alikuwa hanipikii chakula. Imefanyika kama mwaka moja hivi. Ata ukitoka kazi hashughuliki, labda uende hotelini ukule huko," Nyongesa alisema.

Aliendelea kusimulia yaliyotokea mnamo siku ambaye mkewe alichukua mtoto wao mdogo na kutoroka.

"Nilitoka kazi kitu saa kumi na moja. Nikanunua vitu za nyumba, kufika kwa nyumba akaniuliza mambo ya mahindi. Akawa anarusha maneno. Akaniweka kidole kwa macho. Nikamwambia ni heri atoke ama nitoke. Akaenda kwao. Alibeba mtoto wa mwaka mmoja. Huwa tunazungumza. yeye ni mzaliwa wa mwisho kwao, ata akifanya makosa inakuwa ni yangu tu," alisema.

"Majukumu yake ya mwanamke kwa nyumba hafanyi. Ata ukitoka kazi hataki kujua kama umetoka kushughulikia familia ama nini. Alitoka na mimi pia nikatoka. Nilienda kwa familia yetu wiki mbili," aliongeza.

Kwa bahati mbaya, juhudi za kumpatanisha Nyongesa na mkewe hata hivyo hazikufua dafu kwani Bi Josylynn hakupatikana kwa simu.

Nyongesa alipopewa nafasi ya kuzungumza naye hewani, alisema, "Arudi chini, tufunze watoto, aache kukaa na kampuni mbaya, aache kuskiliza watu wa kwao. Ata mimi nikiongea hanichukulii kama mtu. Familia yake inamlinda."

Je, maoni yako kuhusu Patanisho ya leo ni yepi?