Patanisho: Jamaa aliyeshawishiwa na mkewe kuacha kazi ili wakae pamoja arukwa hewani

"Huyo simjui!" Daisy alisema kabla ya kukata simu.

Muhtasari

•Siku ziligeuka kuwa wiki na wiki zikawa miezi huku Korir bado akisubiri mpenzi wake arejee  lakini haikuwahi kutokea.

•Korir alieleza wasiwasi wake kuwa huenda Daisy tayari amepata mtu mwingine na ndio sababu bado hajarejea.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Martin Korir ,24, kutoka Iten alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mpenzi wake Daisy Cherop.

Katika maelezo yake, alisema mkewe alienda kwao Januari mwaka huu na hajawahi kurudi hadi leo. Kabla ya kutengana, wawili hao walikuwa wamekaa pamoja kwenye ndoa kwa takriban miaka miwili.

"Aliniambia anaenda kusalimia mamake. Alisema anaenda wiki moja kisha arudi. Wiki iliisha nikamuuliza kama anakuja akasema mamake ni mgonjwa. Nilisema nisuburi mpaka mama yake apone," alisema.

Siku ziligeuka kuwa wiki na wiki zikawa miezi huku Korir bado akisubiri mpenzi wake arejee  lakini haikuwahi kutokea.

"Alianza kunidanganya kuwa mamake bado ni mgonjwa, nimengoja sana mpaka sasa nimechoka. Nashangaa jinsi alienda akabadilika. Kila wakati nikimuuliza ikiwa atarudi anasema atakuja tu.  Alisema ningoje mpaka Desemba ndio atakuja tukae," alisema.

Korir alieleza wasiwasi wake kuwa huenda Daisy tayari amepata mtu mwingine na ndio sababu bado hajarejea.

Daisy alipopigiwa simu alisema kuwa hamfahamu Martin Korir.

"Huyo simjui!" alisema kabla ya kukata simu.

Martin ambaye alisikika ameumia sana moyoni aliweka wazi kwamba ana uhakika sauti iliyosikika kwenye redio ni ya Daisy na kudokeza kuwa alikuwa akidanganya. 

"Ananijua vizuri sana. Nataka nijue msimamo wake tu" alisema.

Aliongeza "Amenihangaisha sana mpaka nakonda. Nilikuwa nafanya kazi Nairobi. Siku moja alinipigia simu akaniambia niende nyumbani tuanze maisha na yeye. Niliacha kazi nikaenda tukakaa na yeye. Tulikaa na yeye mwaka moja alafu tukaanza kusumbuana kidogo kidogo."

Alipopewa nafasi ya kujieleza kwa Daisy kwenye radio, Korir alimhakikishia mpenziwe kuhusu upendo wake mkubwa kwake na kumuomba arudi nyumbani ili waweze kuendelea na maisha yao pamoja.

Gidi alimshauri Korir akule ili aache kukonda.