Patanisho: Jamaa amfungia mkewe nje usiku baada yake kukosa kumpikia chakula cha jioni

Muhtasari

•Jane alisema mumewe alighadhabika sana baada ya kuamka na kupata  chakula bado hakijawa tayari. 

•Ayub alisita kumsamehe Jane huku akisisitiza kuwa ni sharti aende nyumbani kwake ili kwanza washiriki mazungumzo ya moja kwa moja.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Jane Esokoma ,25, alituma ujumbe alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Ayub Simiyu ambaye walikosana naye kufuatia ugomvi wa kinyumbani.

Mama huyo wa mtoto mmoja alisema ndoa yao ya miaka mitano ilisambaratika mwezi Julai mwaka jana baada ya mumewe kurejea nyumbani na kupata bado hajapika.

"Nilifika nikiwa nimechelewa. Nilikuwa nabomoa nywele. Alifika kwa nyumba akaanza kugombana nami. Aliniuliza mbona sipiki nikamwambia bado ni mapema. Niliendelea kubomoa nywele akaenda kulala. Baada ya muda aliamka akanipata bado nabomoa nywele," Jane alisimulia.

Jane alisema mumewe alighadhabika sana baada ya kuamka na kupata  chakula bado hakijawa tayari. 

Kuona hivyo mwanadada huyo aliamka na kuenda jikoni kuandaa chakula ila mumewe akamfuata na kuzima moto ule kutumia maji.

"Nilitoka nje nikaenda jikoni akaja akamwaga maji kwa moto. Niliwasha moto tena akaja akamwaga maji tena. Nikawasha mara ya tatu akafanya vilevile. Alinifungia nje mpaka saa tisa usiku," Alisema.

Ayub alipopigiwa simu alisita kumsamehe Jane huku akisisitiza kuwa ni sharti aende nyumbani kwake ili kwanza washiriki mazungumzo ya moja kwa moja.

Alitilia shaka ahadi ya mkewe kuwa angeepiga hatua ya kurudi huku akifichua kuwa amewahi kuahidi tena kurudi ila hakurudi.

"Unasema hivo hapo lakini najua hutakuja. Kama unataka msamaha njoo uniombee nyumbani sio hapo kwa redio. Amesema mara mingi atakuja alafu hakuji," Ayub alisema.

Ayub alimsihi mkewe arudi ili waendelee kulea mtoto wao pamoja. Jane alimhakikishia Ayub kuwa bado anampenda na kumuahidi kuwa angerudi ili waweze kuendelea kuishi pamoja..