Patanisho: Jamaa amlaumu mkewe baada ya kufumaniwa kitandani na shemeji yake

Kelvin alidai alianguka kwenye mtego wa kulala na dadake Lucky kwa kuwa waliachwa nyumbani pekee yao.

Muhtasari

•Lucky alisema aligura ndoa yake ya miaka mitatu baada ya kumfumania mumewe kitandani na dada yake mdogo.

•Kelvin alidai kwamba alikuwa amemwagiza mkewe kuenda nyumbani  na dadake ila akakaidi na kuenda pekee yake.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Bi Lucky kutoka Kiambu alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Kelvin ambaye walitengana naye mwaka wa 2020.

Mama huyo wa watoto watatu alisema aligura ndoa yake ya miaka mitatu baada ya kumfumania mumewe kitandani na dadake mdogo.

"Siku moja nilipata habari kuwa mamangu ni mgonjwa. Nilikuwa naishi na dadangu nikamwambia kuwa naondoka kuenda kuona mama.  Baada ya siku tatu niliambia mume wangu anitumie nauli nirudi lakini akasema nisubiri," alisema.

Aliongeza,"Nilitoa pesa yangu mfukoni nikarudi. Kufika nilipata akifanya mapenzi na dada yangu mdogo kitandani."

Lucky alifichua kuwa baada ya kupatikana, mumewe aliondoka mwenyewe na kumuacha na watoto wao watatu.

"Baada ya kufanya kitendo kile dadangu alirudi kijijini. Mume wangu bado hajaoa mwingine. Huwa siongei na yeye.  Mimi niliamua nikae huku kwa sababu najua nikienda nyumbani tutakosana bure," alisema.

Kelvin alipopigiwa simu alibainisha kuwa suala la kurudiana na mama huyo wa wanawe sio rahisi kwa sasa. Alidai ingawa bado hajapata mwingine, anahitaji muda wa kufikiria kwa kuwa ni muda mrefu tangu alipotengana na Lucky. 

"Kurudiana itakuwa ngumu kidogo kwa sababu uliniambia umepata mtu mwingine. Sasa sijui unanitafuta kwa nini," alimwambia mkewe.

Katika utetezi wake, Kelvin alidai kuwa alianguka kwenye mtego wa kulala na dadake Lucky kwa kuwa waliachwa pekee yao nyumbani.

Alidai kwamba alikuwa amemwagiza mkewe kuenda nyumbani pamoja na dadake ila akakaidi na kuenda pekee yake.

"Mimi namlaumu kwa sababu nilimpatia pesa ya watu wawili . Alisema ataenda mwenyewe kwa sababu nauli ingeweza kupanda wakati wa kurudi.  Yeye aliniachia dadake kwa hizi nyumba ambayo ni single," alisema.

Aliongeza, "Anipee muda kiasi nifikirie, sina mke mwingine. Naomba anipatie muda wa kama mwaka moja hivi."

Lucky alisistiza kuwa angependa kurudiana na mumewe licha ya yote yaliyotokea kwa kuwa bado anampenda sana.

"Wacha nifikirie alafu nitakupigia simu. Kutoka niende sijawahi kupata msichana mwingine kama wewe." Kelvin alimwabia Lucky.

Je, una ushauri upi kwa Kelvin na Lucky?