Patanisho: Msichana wa miaka 17 ajuta kuolewa, amuomba mamake amkubali nyumbani

"Huyo jamaa anafaa akamatwe. Huyo mtoto nampenda. Mimi nilitaka asome" Mama Gloria alisema.

Muhtasari

•Gloria alifichua kuwa alitoroka nyumbani mwezi Januari na kuenda kuolewa bila kuwaarifu wazazi wake.

•Mama Gloria alikiri kuwa amekuwa na wasiwasi mwingi tangu bintiye alipotoroka kwani hakufahamu aliko.

GHOST NA GIDI STUDIONI
GHOST NA GIDI STUDIONI GHOST NA GIDI STUDIONI
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Gloria Muhonja alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mama yake Bi Ezires.

Gloria alifichua kuwa alitoroka nyumbani mwezi Januari na kuenda kuolewa bila kuwaarifu wazazi wake.

"Hakuna kitu ilinitorosha nyumbani. Mimi mwenyewe ndo niliamua kutoroka. Tuliishi na yeye (mumewe) kutoka Januari hadi mwezi wa saba. Tuliachana alafu nikarudi nyumbani. Nilitoroka tena nikaenda kuishi na jamaa huyo tu," Gloria alisema.

Alifichua kuwa bado alikuwa katika kidato cha pili wakati aligura nyumbani kwao na kuenda kuolewa.

Mapema mwezi huu aliporudi nyumbani kwao alimdanganya mamake kuwa alikuwa akiishi na rafiki yake wa kike.

"Niliogopa kumwambia mama kuwa nimeoleka. Nilimwambia naishi na rafiki yangu fulani," Alisimulia.

Bi Ezires alipopigiwa simu, Gloria alimjulisha kuhusu nia yake ya kuomba msamaha huku akitetea hatua yake ya kugura nyumbani kwa mara ya pili.

"Mum najua nimekosa na nataka kuomba msamaha. Vile uliniambia nirudi na nikarudi, ulipoenda kazini baba aliniambia ati hanitaki kwa nyumba," Gloria alisema.

Mama Gloria alikiri kuwa amekuwa na wasiwasi mwingi tangu bintiye alipotoroka kwani hakufahamu aliko.

"Nimejaribu kukutafuta mpaka kwa simu sikupati. Mimi sina maneno na wewe. Nimekusamehe kama mama na nimeshau yaliyopita. Ninataka urudi Gloria. Mimi ata sina amani kwa sababu sijui uliko... Mimi nakupenda, urudi nyumbani kwa baba na mama.. Ata wazazi wananiuliza mtoto wangu anaishi wapi. Uliporudi nilikuwa nimefurahi," Mama Gloria alisema.

"Huyo mtoto alikuja nyumbani. Hiyo Jumapili nilikuwa naenda kazini, nilimwambia ningerudi Jumamosi tuongee. Jumatatu nilipigiwa simu nikaambiwa Gloria hayuko," Aliambia Gidi.

Gidi alimfichulia Mama Gloria kuwa bintiye amekuwa kwenye ndoa tangu alipotoroka nyumbani mapema mwaka huu.

Mama Gloria ambaye alisikika kuwa na wasiwasi alikiri kwamba hana taarifa zozote kuhusu kuoelewa kwa binti yake.

"Saa hii ndo ako na miaka 17. Anafaa kuwa katika kidato cha tatu... Huyo jamaa anafaa akipatikana akamatwe. Huyo mtoto nampenda. Mimi nilitaka asome" Alisema.

Gidi alimshauri Gloria kutokimbilia ndoa na badala yake kurudi shuleni ili kukamilisha masomo yake kwanza.

"Usikimbilie ndoa. Kwanza unafaa kurudi shule umalize masomo. Ningeomba urudi nyumbani msuluhishe matatizo yaliyopo," Gidi alishauri.

Gloria alifichua kuwa kwa sasa ndoa yake na mpenziwe mwenye umri wa miaka tayari  imevunjika.

"Mama nataka unisamehe nirudi nyumbani. Naomba usinikatae," Gloria alimsihi mamake.

Mamake alimhakikishia kuwa yupo tayari kumpokea na hata kuahidi kumtumia nauli ya kurudi nyumbani.