Patanisho: Mwanadada amshtaki shemeji kwa baba mkwe baada ya kumtongoza

Doreen alisema shemejiye alimuonya dhidi ya kuambia yeyote kuhusu suala hilo, na kumuomba aweke uhusiano wao "chini ya maji"

Muhtasari

•Doreen alisema uhusiano wao uliharibika baada ya yeye kumshtaki shemeji huyo wake kwa baba mkwe kwa madai ya kumtongoza.

•Hata hivyo, alidai kuwa uhusiano wake na shemejiye ulikiwa mazungumzo tu na kubainisha kuwa hakuwa wameshiriki mapenzi.

Ghost na Gidi
Ghost na Gidi
Image: RADIO JAMBO

Mwanadada aliyejitambulisha kama Doreen Nafula ,26, kutoka kaunti ya Bungoma alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na shemeji yake George Lucas ambaye alikosana naye Disemba 2023 kufuatia masuala ya kinyumbani.

Doreen alisema uhusiano wao uliharibika baada ya yeye kumshtaki shemeji huyo wake kwa baba mkwe kwa madai ya kumtongoza.

Alisema shemeji huyo wake alikuwa amemuonya dhidi ya kuambia yeyote kuhusu suala hilo, ila akakaidi na kumwambia baba mkwe.

"Kuna shemeji yangu ako tu Nairobi. Tulijuana naye mwaka2017 juu kuna wakati mzee alikuwa ameshikwa akaja kumtoa juu ni kakake.   Yeye ni afisa wa polisi.

Shemeji ndiye alishughulikia bwanangu mpaka akatoka,. Yeye ndiye alikuwa anatushughulikia mpaka chakula kwa nyumba. Alianza kunikatika. Akaniambia tucheze chini, hiyo mambo mtu yeyote asijue," Doreen alisimulia.

Aliendelea, "Vile nilienda kutembea ushago, hiyo stori nikaitoboa. Huwa anapewa leave Disemba ndipo akaenda nyumbani akasomewa na wazee Alikalishwa chini na wazee wakamuuliza kwa nini anakatia ndugu ya kakake. Yeye ni binamu wa bwanangu. Baadaye alinipigia simu baada ya kutoka nyumbani akiwa amekasirika sana. Saa hii ata ameniblock,"

Doreen alifichua kwamba baada ya shemeji yake kukalishwa chini na wazee, baba mkwe alimuonya dhidi ya kumwambia mume wake akisema hatua hiyo huenda ikaleta maneno katika familia.

Hata hivyo, alidai kuwa uhusiano wake na shemejiye ulikuwa mazungumzo tu na kubainisha kuwa hakuwa wameshiriki mapenzi.

"Tulikuwa tumeongea ongea, hadi ananiletea shopping. Hatukushiriki mapenzi, ilikuwa tu kuongea kwa simu. Nilikasirika juu hakutaka mtu yeyote ajue. Nataka  tu tukuwe na uhusiano mzuri kama kitambo," alisema.

Bw Lucas alipopigiwa simu, aliskikika kuwa katika nafasi ambayo hangeweza kuzungumza na akasema, "Niko bize sana" kabla ya kukata simu.

Doreen alipopewa nafasi ya kuomba msamaha hewani, alisema, "Shemeji mimi nilikukosea kukusema kwa baba mkwe, naomba unisamehe tuanze ukurasa mpya."

Aidha, alibainisha kuwa hakuna shida iwapo mumewe atajua, kwani kulingana naye, hakuna kitu kibaya kilichotokea.

Je, una maoni yepi kuhusu Patanisho ya leo?