Patanisho: Mwanadada amuacha jamaa na mtoto aliyeolewa naye, atoroka na waliyepata pamoja

Wambui alimshtumu David kwa kutoka kimapenzi na aliyekuwa mpenzi wa baba yake.

Muhtasari

•David alisema Wambui aligura ndoa yao ya miaka miwili mwaka wa 2019 baada ya kupatikana akitoka nje ya ndoa.

•Wambui alipopigiwa simu aliweka wazi kuwa hana nia ya kurudiana na David.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, David Matandi alituma ujumbe akiomba kusaidiwa kupata suluhu ya mzozo wa watoto kati yake na aliyekuwa mpenzi wake Maria Wambui.

David alisema Wambui aligura ndoa yao ya miaka miwili mwaka wa 2019 baada ya kupatikana akitoka nje ya ndoa.

"Tulikuwa tumeoana naye.  Baada ya miaka mbili alianza kutoka nje ya ndoa. Alipoona ni kama najua aliondoka akaniachia mtoto mmoja alafu akaenda na mwingine. Mtoto aliyeacha alikuwa na miaka miwili," alisema.

David alifichua kuwa mpenziwe huyo wa zamani alimwachia mtoto aliyekuja naye na kumbeba yule waliyempata pamoja.

"Kila wakati nikipiga simu huwa ananitusi. Nikimwambia nimpelekee mtoto anasema hamtaki," alisema.

Alisema kuwa Wambui amekataa katakata kurejesha mtoto wao na kubainisha kuwa hataki mtoto ambaye aliacha.

"Anasema anataka huyo ambaye tulipata na yeye. Baba ya huyu tuliye naye ako lakini simjui. Alikuja na ujauzito akazalia kwetu. Nataka akuje achukue mtoto ama alete huyo mwingine niwalee wote wawili," alisema.

Wambui alipopigiwa simu aliweka wazi kuwa hana nia ya kurudiana na David. Hata hivyo alisema yupo tayari kumchukua mtoto ambaye alimwachia mzazi huyo mwenzake.

Wambui hata hivyo alikanusha madai ya kuenda nje ya ndoa na badala yake kumshtumu David kwa kuoa mpenzi wa baba yake.

"Alichukua msichana ambaye alikuwa ameolewa na baba yangu wakakakaa na yeye.  Yeye mwenyewe alinipigia simu akaniambia kuwa ashaoa mwingine nisishinde nikirudi tena. Mimi kurudiana naye siwezi," alisema.

David alidai kuwa mama huyo wa mwanawe amekuwa akitumia wanaume kumshambulia kila anapoenda kuchukua mtoto wake.

Alisema kuwa wanaume hao ambao alidai kuwa ni wapenzi wa Wambui wamewahi kumpiga mara kadhaa.