Patanisho: Peace asikitika baada ya mumewe, Amani kuhama na kumuacha akiwa mjamzito

"Sasa mimi nitakula nyumbaambayo utajenga ama?" Peace alihoji.

Muhtasari

•Peace alisema kuwa mumewe aliondoka nyumbani ghafla mwezi Januari bila kumueleza  na hajawahi kurudi tangu wakati huo.

•Bw Amani aliweka wazi kwamba anapanga kurudi nyumbani mwezi Aprili ili aweze kujenga nyumba ambako wataishi.

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Katika kitengo cha Patanisho, Peace mwenye umri wa miaka 23 alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Milk Zedek Amani.

Peace alisema kuwa mumewe aliondoka nyumbani ghafla mwezi Januari bila kumueleza  na hajawahi kurudi tangu wakati huo.

"Ilikuwa mwezi Januari ambapo alitoweka. Nilikuwa nimeenda kazini kurudi kwa nyumba nikapata hayuko. Nilipata amechukua nguo zake kadhaa. Nilipomuuliza alisema ameenda kazi," Peace alisimulia.

Aliendelea, "Nilijaribu kumuuliza ameenda kazi gani na wapi lakini hakuniambia. Nilijaribu kuwaambia wazazi wake lakini anasema tu yuko kazi. Sijajua kazi ambayo alienda. Hajawahi kurudi nyumbani."

Mwanadada huyo alisema kwa sasa ana ujauzito wa miezi mitano na akabainisha kuwa mume wake Bw Amani anafahamu hilo.

"Anasema ko kazi atarudi. Anajua niko na mimba. Nataka nijue amefanya uamuzi gani. Tumekaa kwa ndoa miaka mitatu," alisema.

Bw Amani alipopigiwa simu alitupilia mbali madai ya kugura ndoa yake na kumuacha mkewe akiwa mjamzito.

Amani alieleza kwamba alilazimika kuhamishwa kazi kwa kuwa mahali ambapo alikuwa hakuwa anavuna za kutosha.

"Mimi sijaenda zangu. Nilimwambia naenda kazi. Mahali nilikuwa nafanya pesa haikuwa inatosha.  Walinihamisha nikaenda Kakamega. Tunakaa na rafiki yangu," Amani alisema.

Bw Amani aliweka wazi kwamba anapanga kurudi nyumbani mwezi Aprili ili aweze kujenga nyumba ambako wataishi.

Peace hata hivyo alipingana na mipango ya mumewe huku akifichua kwamba hajakuwa akimsaidia katika mahitaji yake.

"Alituma tu shilingi mia tatu mwezi moja... Wewe ungesema wamekupiga transfer na ningeelewa. Sasa mimi nitakula nyumba utajenga ama?" Peace alisema.

Peace alimbainishia mumewe kwamba kwa sasa hawezi kuenda kazini kwa kuwa ujauzito wake ni mkubwa. Hata hivyo alimhakikishia kwamba bado anampenda na kumuomba aanza kushughulikia mahitaji yake.

"Amani mimi nakupenda kama nyama choma lakini wewe ushughulike," alisema.

Amani aliahidi kurudi nyumbani mwezi ujao.