Patanisho: Wafula amwadhibu mkewe kwa kumfunga mikono juu ya nyumba kwa saa 3 asiweze kuketi

Wafula alimshtumu mkewe kwa kuchukua vitu vya nyumba vikiwemo jiko, thermos, vikombe na kuuza bila idhini yake.

Muhtasari

•Wafula alisema ndoa yake ya miaka saba ilisambaratika wakati mama mkwewe alimkujia bintiye baada ya kupata taarifa kuhusu jinsi ambavyo alimtesa.

•Doreen alipopigiwa simu aliweka wazi kuwa hataki kabisa kurudiana na mzazi huyo mwenzake kutokana na mateso aliyomfanyia.

Image: RADIO JAMBO

Emmanuel Wafula ,30, kutoka Webuye alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Doreen Nandako ,23, ambaye alimuacha baada ya kumpa adhabu ya kikatili.

Wafula alisema ndoa yake ya miaka saba ilisambaratika wakati mama mkwewe alimkujia bintiye baada ya kupata taarifa kuhusu jinsi ambavyo alimtesa.

"Sikumpiga lakini adhabu ambayo nilimpea niliona sikufanya vizuri. Niliogopa kumpiga lakini nikamfunga mkono asikae chini. Nikamfunga kwa nyumba juu ya ili akitaka kuketi ananing'inia hawezi kukaa chini. Nilimfunga kitu saa tatu nikamfungua saa tisa. Kuna kitu ilikuwa inaniuma roho wakati nilimuadhibu," Wafula alisimulia.

Aliendelea, "Ilifika mahali mke wangu alikuwa anachukua kitu kwa nyumba anapeleka mahali. Nikimuuliza anafura. Kumbe anapeleka kuuza na haniambii. Kuna wakati alisema mama yake anataka cooker nikamwambia kama ni mama yake anataka ni sawa. Mama yake hata hivyo alikana. Aliendelea kuchukua thermos, vitu kwa nyumba na ukimuuliza ananuna tu. Kuna kipindi shule zilifungwa, akapotea wiki mbili akazima simu. Kurudi akaniambia alikuwa ameenda kazi. Hii adhabu nilikuwa nampa nikimwambia aombe msamaha. Alikuwa anasema afikirie kama ataomba msamaha. Nilimwambia acha nimpee adhabu initoke kwa roho. Kesho yake alimuambia mama yake. Kibaya nilichofanya, wakati nilimfunga nilipiga picha. Alionyesha mama yake picha wakatuma gari akachukuliwa."

Wafula alieleza kuwa juhudi zake kumfuatilia mkewe ili arudi hazijaweza kuzaa matunda, jambo ambalo limempelekea kuleta Patanisho.

"Niliambiwa niandike barua kusema ni mimi niko naye ili tuongee. Walikuwa wanahofia kuna mahali inaweza fika nimuue alafu nikane sio mke wangu. Nilienda kwao nikangoja wataniita. Imepita miezi miwili lakini hawajaniita," alisema.

Doreen alipopigiwa simu aliweka wazi kuwa hataki kabisa kurudiana na mzazi huyo mwenzake kutokana na mateso aliyomfanyia.

"Siwezi nikarudiana na yeye. Siwezi nikajua kama alienda nyumbani akaongea nao. Alinifanyia hivyo mara mbili," alisema.

Kuhusu madai ya kuuza mali ya nyumba, alisema, "Sikuchukua vitu alafu nikauza. Nilikuwa nimeshikika mahali nikamuomba pesa akasema hana. Ilikuwa gas. Sikuuza.. Nilimwambia anipee pesa nimletee."

Patanisho hiyo kwa bahati mbaya haikuweza kuendelea kwani simu ya Doreen ilikatika kisha akazima.

Wafula kwa upande wake alisema ombi lake ni mzazi huyo mwenzake arudi nyumbani ili waweze kulea watoto pamoja.

"Shida ni kwamba nikimpigia simu hashiki. Mimi nilikuwa nataka arudi tulee watoto wetu," alisema.

Kwa kumalizia, Wafula alidai watu wa Webuye wanaomba masaa ya Patanisho yaweze kuongezwa ili wanaoomba kupatanishwa wapate muda wa kujieleza vizuri.

Je, una ushauri gani kwa wawili hao?