Patanisho:"Ukipata pesa unabet, unabet mwaka mzima!" Jamaa azomewa na mkewe, ashinikizwa atoke Nairobi

Elizabeth pia alilalamikia tabia ya mumewe ya kucheza kamari na ya kusikiliza maneno ya watu wengine.

Muhtasari

•Mandela alidokeza kuwa wakati alipokutana na Bi Nangila, mke huyo wake alimdanganya kuhusu idadi ya watoto wake.

•Elizabeth alibainisha kwamba alifikia hatua ya kurudi kwao baada ya kuona maisha ya Nairobi yalikuwa yamewalemea.

•Elizabeth alimhakikishia mumewe kwamba bado amemuweka moyoni na kubainisha kwamba uhusiano wake na mzazi mwenzake uliisha kabisa.

Image: RADIO JAMBO

Bwana Marvin Mandela ,28, alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mke wake Elizabeth Nangila ,30 ambaye alimuacha mwaka jana.

Mandela alisema ndoa yake ya miaka mitano ilisambaratika Novemba mwaka jana wakati ambapo mkewe aliondoka ghafla bila maelezo.

"Nilitoka kazi nikapata ameenda. Niilipompigia simu aliniambia ameenda nyumbani kwa ajili ya shughuli fulani. Hata hivyo, nilipofuatia niliambiwa ameenda kutayarisha watoto wake. Watoto wake wawili walikuwa wanakaa nyumbani kwa mamake. Wakifunga shule walikuwa wanakuja kutembea Nairobi. Tulikuwa tunazungumza kwa simu na nikipata kitu kidogo namtumia ya matumizi akiwa nyumbani kwao," Mandela alisimulia.

Mandela alikiri kwamba aliwahi kumtusi mkewe na kumpiga mara moja, jambo ambalo huenda lilimkasirisha na kufanya atoroke.

Aidha, alidokeza kuwa wakati alipokutana na Bi Nangila, mke huyo wake alimdanganya kuhusu idadi ya watoto wake.

"Wakati tulipatana aliniambia ako na mtoto mmoja. Nilipofuatilia nilijua ako na watoto wawili vijana. Wakati akienda, kuna watu aliniambia anarudi kwa bwanake. Nataka anieleze ukweli nijue ili niendelee na maisha yangu. Kuna watu aliambia amerudi kwa bwana yake. Nataka nijue kama ni ukweli. Tulipokuwa naye alikuwa anaongea na baba wa watoto wake na nikimuuliza anakuwa mkali," alisema.

Elizabeth alipopigiwa simu aliweka wazi kwamba amekuwa nyumbani kwao tu baada ya kugura ndoa yake mwaka jana.

Elizabeth alibainisha kwamba alifikia hatua ya kurudi kwao baada ya kuona maisha ya Nairobi yalikuwa yamewalemea.

"Mimi si nilishakwambia maisha ya Nairobi siwezani nayo. Nilikwambia tumeishi Nairobi muda mrefu na hatuoni mafanikio. Nilikwambia tujaribu tutoke Nairobi tujaribu maisha ya nyumbani. Niliona nyumbani kwetu angalau waliniachia shamba kidogo, ndio natumia kupanda miwa. Tayari nimevuna na hata nikanunua kondoo wawili," Elizabeth alisema.

Aliongeza, "Hali yako ni ya uongo. Hakuna kitu unaahidi alafu unatimiza. Nilifungua biashara ukaangusha. Tukafungua hoteli ikaanguka. Niliona nitoke niende niishi nyumbani ndio ufungue macho uone bibi yako ameenda kwa nini. Maisha ya Nairobi imekushinda na umekwama huko. Kama ni upendo nilishakumwagia  wote. Babako alikufa akakuacha na mashida. Biashara ikikushida, Nimejaribu kukushauri husikii."

Elizabeth pia alilalamikia tabia ya mumewe ya kucheza kamari na ya kusikiliza maneno ya watu wengine.

"Wewe ukipata pesa unabet, unabet the whole year. Nimejaribu kukusaidia husaidiki. Utashinda maisha ya kuomba? Mimi sipendi maneno ya kuambiwa na majirani. Mimi nimeishi nyumbani. Sijawahi kutoka kwetu tangu nitoke Nairobi. Wewe shinda Nairobi na kubet. Nimejaribu sana kukuambia uache hutaki."

Elizabeth alimhakikishia mumewe kwamba bado amemuweka moyoni na kubainisha kwamba uhusiano wake na mzazi mwenzake uliisha kabisa.

"Bado hujatoka akilini mwangu, wewe bado ni mume wangu. Nilikuelezea. Yule anaendelea na maisha yake, ako na bibi na mtoto," alisema.

Mandela alisema, "Mimi nimepata ukweli, bado nakupenda. Mambo yote ambayo tumeongea nitarekebika na nakupenda sana."

Kwa upande wake, Elizabeth alisema, "Jaribu tu uwezavyo wakati usiachwe nyuma maishani. Fungua macho tuwe tumesaidika maishani. Nilikwambia mimi sifurahii vile nakaa kwetu.Na bado niko na wewe. Nilikwambia sitawahi kurudi na mume wangu. Acha kusikiliza maneno ya majirani, mimi bado nakupenda."

Je, ushauri wako kwa wawili hao ni upi?