"Unataka kumnyang'anya Massawe Customers" Gidi amuonya mwanadada aliyetaka kummulika mumewe

Gidi alihofia kumtafuta Kevo kufuatia masaibu ya awali wakati akishughulika na wengine wenye jina hilo.

Muhtasari

•Jerida alisema ndoa yao ya miaka saba imejaa misukosuko na wamekuwa wakikosana mara nyingi hadi akafikia hatua ya kuenda nyumbani kwao.

•Kelvin alipopigiwa simu hata hivyo, alibainisha kwamba hana shida na mkewe na kumwagiza arudi nyumbani

Gidi na Ghost
Gidi na Ghost
Image: RADIO JAMBO

Jerida Imbosa ,27, kutoka Mumias alituma ujumbe akiomba kupatanishwa na mume wake Kevin Onema ,32, ambaye alikosana naye mwezi mmoja uliopita.

Jerida alisema ndoa yao ya miaka saba imejaa misukosuko na wamekuwa wakikosana mara nyingi hadi akafikia hatua ya kuenda nyumbani kwao.

Alifichua  kwamba hawakubahatika kupata mtoto katika kipindi cha miaka saba ya kwanza ya ndoa yao na kumfanya mumewe kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje hadi akazaa na mwanamke mwingine.

"Alinioa tukakaa miaka saba kama hatujajaliwa mtoto. Akaanza kuenda nje ya ndoa. Akapata mtoto huko nje akaanza madharau. Siku moja alipanga niende kwa mwanafamilia wao mmoja ndio mtoto akaletwa kwa nyumba akanyolewa na mamake," alisimulia.

Aliongeza, "Mwaka jana mwezi wa Aprili nikajaliwa na mtoto wangu. Hata hivyo aliendelea na madharau. Tukiwa tunalala usiku kazi yake ni kuongea tu na wasichana.Nilisema niende nyumbani nitulize akili. Sasa nikimpigia simu anasema niache kumsumbua. Ata mtoto mwenyewe hataki kumsaidia."

Jerida alimuomba mtangazaji Gidi amshurutishe Kelvin kusaidia mtoto wao hata ikiwa hatakubali warudiane.

Mwanzoni, Gidi alisita kwa kuwa alihisi kama kwamba Jerida alitaka kummulika mumewe kwa kutowajibikia mtoto, ambalo sio lengo la kitengo cha Patanisho.

"Hiyo sio kazi yetu, ni kazi ya Massawe. Lengo la Patanisho ni kuwapatanisha wawili ambao wamekosana. Hii ni Massawe kushughulika naye. Wewe unataka kunyang'anya Massawe Customers," Gidi alimwambia Kelvin.

Aidha, mtangazaji huyo alihofia kumpigia Kevo kufuatia masaibu ya awali wakati akishughulika na wengine wenye jina hilo.

Kelvin alipopigiwa simu hata hivyo, alibainisha kwamba hana shida na mkewe na kumwagiza arudi nyumbani

"Si arudi, kwani kuna shida gani," alisema kabla ya kukata simu.

Gidi alijaribu kumshauri Jerida aachane naye kwa kuwa alionyesha kutojali ila mwanadada huyo akasisitiza atafutwe tena.

Alipopigiwa tena, Kelvin alimwambia Jerida, "Wewe huna kazi ya kufanya. Nilikwambia ufanye shughuli zako mwenyewe. Unaomba msamaha kwani ulikosea nini. Nilikwambia wewe urudi mwenyewe."

Alimwambia Gidi amwagize mkewe arudi mwenyewe kwani hakumfukuza nyumbani.

"Yeye arudi ndiye anachelewa. Ile shida nilikuwa nayo mama alimaliza," alisema.

Jerida alisema yuko tayari kurudi ila akamuomba mzazi huyo mwenzake arekebishe tabia zake.

Gidi aliwashauri wapenzi hao waweze kuketi chini ili kusuluhisha mzozo wao na kuwaomba washirikishe wazazi.