In Summary

•Mwanablogu huyo ambaye ametangaza nia ya kuwania kiti cha urais miaka ya usoni alikiri kuwa pia yeye ako na marafiki wengi wa jamii ya LGBT na akasihi Wakenya kuwachukulia kwa usawa.

•Dela alitangaza kuwa jumbe alizokuwa anapokea zilikuwa nyingi kiasi kuwa alishindwa kabisa kulala.

Xtian Dela
Image: Instagram

Mwanablogu Aurther Mandela almaarufu kama Xtian Dela amelalamika kupokea jumbe za chuki kutoka kwa Wakenya kutokana na msimamo wake kuhusiana na mashoga, wasagaji, wanaovutiwa kimapenzi na jinsia za kiume na kike na watu wenye sehemu za siri za kiume na kike pamoja almaarufu kama LGBT.

Kupitia mtandao wa Twitter siku ya jumanne, Dela alitangaza kuwa jumbe alizokuwa anapokea zilikuwa nyingi kiasi kuwa alishindwa kabisa kulala.

"Nimekuwa nikipokea maoni ya chuki, kupigiwa simu, barua pepe na nakala za chuki siku nzima kutokana na msimamo wangu kuhusiana na LGBT. Matusi, chuki na machungu yale ni mengi sana kiasi kwamba sijaweza kulala. Uonevu wa kimitandao ninaopokea umekithiri. Chuki kubwa sana kwa jamii ya LGBT." Dela aliandika.

Siku ya Jumapili Dela alikuwa amewahimiza wanajamii ya LGBT kubadilisha maeneo yao ya upigaji kura wahamie eneo bunge la Westlands ili wamsaidie kunyakua kiti cha ubunge eneo hilo huku akiwaahidi kutetea haki zao bungeni akichaguliwa.

"Ni wakati sisi kama Wakenya tukubali kuwa kuna watu wengi sana wa jamii ya LGBTQI nchini na tupitishe sheria za kuwalinda badala ya kuwasuta na kuwatusi. Mimi mwenyewe sina shida nao mbona tusiwalinde hadharani na kisheria?" aliandika Dela kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mwanablogu huyo ambaye ametangaza nia ya kuwania kiti cha urais miaka ya usoni alikiri kuwa pia yeye ako na marafiki wengi wa jamii ya LGBT na akasihi Wakenya kuwachukulia kwa usawa.

"Watu wanafaa kuwa huru kupenda yeyote ambaye wanataka kupenda kibinafsi ama hadharani! Mapenzi ni mapenzi ni wakati Kenya ikubali hilo" Dela alisistiza.

View Comments