In Summary

•Eric amedai kuwa lengo kuu la Wanjigi ni kuhakikisha kuwa Kenya imejikwamua kutoka kwenye pango la madeni na kuhakikisha kuwa kila Mkenya ameweza kutia pesa mfukoni.

•Omondi amembubujikia bwenyenye huyo sifa tele na kuwashawishi Wakenya kumpigia kura ifikiapo mwaka ujao akidai kuwa tofauti na wagombeaji wengine wa kiti cha urais, Wanjigi hajawahi kuwa kwenye ulingo wa siasa.

Image: INSTAGRAM

Licha ya kukemewa na wanamitandao baada ya kumpendekeza bwenyenye Jimi Wanjigi kuwa rais wa Kenya mwaka ujao, mchekeshaji Eric Omondi ameendelea kumpigia debe mfanyibiashara huyo.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, msanii huyo mwenye umaarufu mkubwa nchini na kote bara Afrika amesema kuwa alishiriki mazungumzo na mgombeaji  huyo wa kiti cha urais na tikiti ya ODM kuhusiana na maono na mipango yake kwa taifa.

Eric amedai kuwa lengo kuu la Wanjigi ni kuhakikisha kuwa Kenya imejikwamua kutoka kwenye pango la madeni na kuhakikisha kuwa kila Mkenya ameweza kutia pesa mfukoni.

"Asubuhi ya leo nilipata chamsha kinywa na kushiriki mazungumzo pamoja na rais mtarajiwa wa Kenya mtukufu Jimi Wanjigi katika makazi yake. Alinionyesha maono na mipango yake kwa taifa hili. Kila anachoguza hubadilika kuwa dhahabu!! Kama mfanyibiashara aliyefanikiwa zaidi nchini lengo lake ni kuhakikisha kuwa Kenya imejikwamua kutoka kwenye madeni na kuhakikisha kuwa kuna mali na pesa zaidi kwenye mifuko ya Wakenya" Eric aliandika.

Kulingana na msanii huyo, Wanjigi anapanga kutumia ujuzi wake wa biashara kufufua uchumi wa nchi, kutengenezea vijana ajira, kukuza miundombinu, kuleta elimu ya bure na kuwezesha huduma za afya ya bei nafuu.

Omondi amembubujikia bwenyenye huyo sifa tele na kuwashawishi Wakenya kumpigia kura ifikiapo mwaka ujao akidai kuwa tofauti na wagombeaji wengine wa kiti cha urais, Wanjigi hajawahi kuwa kwenye ulingo wa siasa.

"Wanjigi ni  mtu thabiti, mwenye uwezo na asiyetikiswa kama vile mti wa Mugumo. Miongoni mwa wagombea kiti wengine yeye pekee ndiye pumzi ya hewa safi. Wengine wote wamekuwa kwenye siasa bila mengi ya kuonyesha. Kama taifa hatuwezi endelea kufanya kitu kimoja  na kuchagua watu walewale  na kutarajia matokeo tofauti. Ni wakati wa mwanzo mpya!Wakati wa mabadiliko!! Wakati wa Fagia Wote!! Wakati wa Jimi Wanjigi!!" Eric Amesema.

Amewaomba Wakenya kusita kuchagua wanasiasa ambao wamekuwa kwenye siasa kwa miaka mingi wakitarajia mambo mapya kutoka kwao.

View Comments