In Summary

•Melody alisema kabla ya kujitosa kabisa kwenye uimbaji alihusika zaidi katika uandishi wa nyimbo za wasanii wengine.

•Jay Melody aliweka wazi kwamba aliandika kila kitu katika kibao cha  'Njiwa' chake Willy Paul na Nandy.

Jay Melody na Massawe Japanni
Image: RADIO JAMBO STUDIO

Mwimbaji wa Bongo Sharif Said Juma almaarufu Jay Melody amefichua kwamba amewahi kuwaandikia nyimbo wasanii mashuhuri wa Kenya Willy Paul na Nadia Mukami.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha hapa nchini, Melody alisema kabla ya kujitosa kabisa kwenye uimbaji alihusika zaidi katika uandishi wa nyimbo za wasanii wengine.

Alifichua kwamba aliandika nyimbo za Willy Paul 'Hallelujah' na Njiwa pamoja na 'Nitadata' wake Nadia Mukami.

"Nyimbo nyingi nimeandika. Nyingi hazijatoka pia," alisema.

Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 25 alieleza kuwa wasanii wengi walianza kufuata huduma zake za uandishi wa nyimbo baada ya kumwandikia malkia wa Bongo, Nandy wimbo 'Kivuruge' alioachia mwaka wa 2018.

Jay Melody aliweka wazi kwamba aliandika kila kitu katika kibao cha  'Njiwa' chake Willy Paul na Nandy.

"Willy Paul bila shaka alilipa pale THT. Bado nilikuwa THT. Nami nikalipwa kutoka hapo," alisema Melody.

Alifichua kuwa hakuwahi kukutana na Willy Paul uso kwa uso wakati wa mchakato mzima wa kuandika na kuuza maandishi ya muziki.

"'Njiwa' ulikuwa ni wimbo wangu wote. Kila kitu, ilikuwa ni wimbo kamili, vesi ya kwanza na ya pili," alisema.

Ingawa hakutaja kiasi halisi cha pesa alicholipwa, alidokeza kwamba alilipwa hela ambazo zingeweza kumnunulia iPhone.

Melody alisema alifanya uandishi wa muziki kuwa biashara yake kabla ya kupiga hatua kubwa ya kuimba nyimbo hizo mwenyewe.

"Nilikuwa nafanya hivyo ili nipate pesa. Mimi sikuenda kurekodi studio kwa sababu ilikuwa lazima upate nafasi au hela itakayokusaidia kufanya vingine. Wakati huo ilikuwa hata simu sina, kwa hiyo lazima ninunue simu," alisema.

Alifichua kwamba aliweza kununua simu yake ya kwanza baada ya kulipwa kwa kumuandikia Nandy wimbo.

Aidha alisema kwamba aliacha kulalamika kwa kutotajwa na msanii aliyeandikia wimbo na kubainisha kuwa hana kinyongo na msanii yeyote aliyeandikia wimbo.

Katika mahojiano na Massawe Japanni kwenye Radio Jambo siku ya Ijumaa, Melody alifichua kwamba aliwahi kuwaandikia nyimbo wasanii wengi wa Bongo akiwemo bosi wa lebo ya The African Princess, Nandy.

Melody pia alisema kwamba amepata msukumo wa muziki kutoka kwa wasanii kadhaa wa Bongo wakiwemo Ali Kiba na Diamond.

"Napenda wasanii wengi sana. Namtambua Ali Kiba, Lady Jay Dee nyimbo zake ni nzuri, Diamond.." alisema.

Mwimbaji huyo alikubali kuwa Diamond ameendelea kutesa licha ya kuwa kwenye tasnia ya Bongofleva kwa muda mrefu.

Pia alibainisha kuwa nyimbo za Lady Jaydee bado zinaendelea kushabikiwa na wengi licha ya kuwa uimbaji wake umefifia sana kwa sasa.

Nchini Kenya, Melody alisema anawapenda wasanii wengi ambao ameweza kuzoa msukumo mkubwa kwao.

"Nawapenda watu wengi Kenya. Napata msukumo kwa wasanii wa Kenya. Nawapenda kina Otile Brown, Jovial Mejja, Masauti," alisema.

Alisema kuwa nyimbo za Kenya zinachezwa na kupendwa sana nchini Tanzania hasa jijini Dar es Salaam.

View Comments