In Summary

•Jay alisema yupo hai na mwenye afya njema kabisa, na akawataka watu kupuuzilia mbali habari potofu zilizosambazwa mitandaoni.

•Taarifa za uongo zilienezwa kwenye mitandao ya kijamii ikidaiwa kwamba msanii huyo ameaga dunia baada ya kuugua tena.

Mwanamuziki Joseph Haule almaarufu kama Profesa Jay
Image: HISANI

Mwanamuziki mkongwe wa Tanzania Joseph Haule almaarufu Profesa Jay yupo hai na mwenye afya njema, kinyume na uvumi uliosambazwa siku ya Jumatatu.

Msanii huyo aliyegeuka kuwa mwanasiasa alizungumza na gazeti la Tanzania la Mwananchi Leo siku ya Jumatatu ambapo alipuuzilia mbali taarifa za yeye kuaga dunia ambazo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii.

Jay alisema yupo hai na mwenye afya njema kabisa, na akawataka watu kupuuzilia mbali habari potofu zilizosambazwa mitandaoni.

"Mimi niko salama kabisa na hapa nipo nyumbani kwangu nimetulia wala siumwi hata mafua. Naomba hizo habari za kifo kuhusu mimi zipuuzwe kabisa na watu waendelee kusapoti kazi zangu," Profesa Jay alisema Jumatatu.

Aliongeza, "Pia nawaomba Mwananchi mnisaidie kukanusha hili kwa mashabiki zangu, najua mna nguvu kubwa kunisaidia kwenye hili."

Siku ya Jumatatu, taarifa za uongo zilienezwa kwenye mitandao ya kijamii ikidaiwa kwamba msanii huyo ambaye amekuwa kwenye tasnia kwa zaidi ya miongo miwili alikuwa ameaga dunia baada ya kuugua tena.

Haya yalitokea zaidi ya mwaka mmoja baada ya mwimbaji huyo mkongwe kurejea nyumbani kutoka hospitalini ambako alikuwa amelazwa kwa miezi kadhaa.

Mei mwaka jana, Jay alitoa taarifa kuhusu maendeleo ya afya yake baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini ambapo alibainisha kuwa sasa yupo imara na anaendelea vizuri.

Jay alisema kwamba alikuwa katika hali mbaya sana akibainisha kwamba Mungu alimuokoa kutokana na hali hiyo.

"Kwanza namshukuru sana MUNGU aliye hai kwa uponyaji na kunipa nafasi nyingine ya kuendelea kuwa hai, Hali yangu ilikuwa mbaya isioelezeka, Asante sana Mungu baba, nitakutukuza na kukusifu siku zote za maisha yangu," alisema.

Mwanamuziki huyo aliendelea kutoa shukrani za dhati kwa wote ambao walisimama naye katika kipindi cha maumivu yake.

Pia aliwashukuru wahudumu wa afya ambao walifanya juu chini kuhakikisha kuwa afya yake imerejea hasa alipokuwa ICU siku 127.

"Zaidi nawashukuru sana Madaktari na Manesi wote wa muhimbili na kote nilikopitia kwa kunipa matibabu ya kiwango cha juu kwa zaidi ya mwaka mzima niliolala hapo Muhimbili hasa zile siku 127 za hatari nilizokuwa nimelazwa ICU, mlijitoa kwa uwezo wenu wote kuhakikisha kuwa mnaokoa uhai wangu ,AHSANTENI SANA."

Isitoshe, alitoa shukrani za dhati kwa watumishi wa Mungu kwa kumuombea hadi kufikia hatua ya kupata afueni hatimaye.

Aidha, alishukuru familia yake yake kwa ushirikiano mkubwa na upendo walioonyesha wakati wa ugonjwa wake.

View Comments