In Summary

• Katika siku yangu ya kuzaliwa ya miaka 8, nilipimwa rasmi na kukutwa na VVU. Wazazi wangu waliambiwa waende nami nyumbani na WANIPENDE kwa sababu madaktari wangu hawakuwa na uhakika ningeona siku yangu ya kuzaliwa ya miaka 12 - Doreen Moracha.

Jasiri wa kupambana na unyanyapaa wa Ukimwi, Doreen Moraa Moracha
Image: INSTAGRAM

Jasiri wa kupigana dhidi ya unyanyapaa wa virusi vya Ukimwi, Doreen Moraa Moracha mwenye umri wa miaka 30 amefunguka kwamba wazazi wake waliambiwa mwanadada huyo ana virusi vya ukimwi akiwa na umri wa miaka 8, ambapo walisema kwamba hangefika umri wa miaka 12 akiwa na virusi hivyo, lakini miaka 22 baadae, bado yupo hai tena mwenye afya imara kama ukuta wa Berlin.

Akielezea katika ukurasa wake wa Instagram, Moracha alisema kwamba baada ya kupatina na kirusi hicho hatari, wazazi wake waliambiwa warudi naye nyumbani na kumpenda tu kwa kipindi ambacho walikitabiri kuwa chini ya miaka 4 kabla ya kifo chake kutokana na makali ya virusi vya Ukimwi.

Alisema kwamba alizaliwa na virusi hivyo na ndugu yake ambaye kwa sasa ni marehemu waliambukizwa pindi baada ya kuzaliwa na mama yao bila kujua.

“Miaka 22 iliyopita katika siku yangu ya kuzaliwa ya miaka 8, nilipimwa rasmi na kukutwa na VVU. Wazazi wangu waliambiwa waende nami nyumbani na WANIPENDE kwa sababu madaktari wangu hawakuwa na uhakika ningeona siku yangu ya kuzaliwa ya miaka 12. Jambo ni kwamba wakati huo hakukuwa na matibabu, mama yangu alinizaa bila kujua hali yake ya VVU na marehemu kaka yangu na mimi tuliambukizwa,” alielezea Moracha.

Kipindi kile hakukuwa na tiba lakini jasiri huyo wa unyanyapaa aliwashauri watu ambao kwa bahati mbaya wamepatikana na kirusi hicho kutojidharau kwani siku hizi kuna vidonge vya ARV vinavyopunguza makali ya Ukimwi.

“VVU sio tena hukumu ya kifo kama ilivyokuwa zamani. Usiogope kuanza matibabu, unastahili kuishi maisha yako kwa uwezo wake kamili KUMBUKA HAYO! Na sehemu nzuri zaidi ni kwa uzingatiaji sahihi, ukipunguza kiwango cha virusi, huwezi kusambaza VVU kwa ngono. VVU vimebadilika, kwa hivyo badilisha mawazo yako pia,” alitoa ushauri Doreen.

View Comments