In Summary

•Stivo amedai kwamba kuna tabia za Vishenwa ambazo hazikumpendeza na ndiposa akaamua kumtema.

•Msanii huyo alidokeza kwamba amevutiwa na mwanamuziki mwenzake  kutoka Mombasa, Adasa

Image: INSTAGRAM// STIVO SIMPLE BOY

Mwanamuziki mashuhuri kutoka Kibera, Stivo Simple Boy, amethibitisha kwamba hayupo tena kwenye mahusiano na Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy.

Stivo ambaye alipata umaarufu kufuatia kibao chake 'Mihadarati' amedai kuna tabia za Vishenwa ambazo hazikumpendeza na ndiposa akaamua kumtema.

"Siwezi kusahau mahali nimetoka. Lakini ikiwa tabia za mtu hazikupendezi, unasonga mbele na maisha yako," Stivo alisema akiwa kwenye mahojiano na Eve Mungai.

Msanii huyo alidokeza kwamba amevutiwa na mwanamuziki mwenzake  kutoka Mombasa, Adasa. Ingawa hakufichua wazi ikiwa anamchumbia Adasa, Stivo alisema "Wanasema mke mwema hutoka kwa Bwana. Kama mtu amekupendeza, enda naye," alipoulizwa kama wao ni wapenzi.

Adasa alifichua kwamba walijuana takriban mwaka mmoja uliopita baada ya Stivo kumtumia ujumbe kwa minajili ya kikazi.

"Stivo ni mtu ako na vibe, mtu ako roho safi, si mtu ambaye nitasalimia leo kesho basi. Amekuwa rafiki yangu.. tulijuana kikazi. Hata mkituona pamoja ni kazi tu. Mapenzi siwezi kujua, mimi sio Mungu. Huwezi kajua kitakachotokea katika hiyo harakati ya kazi," Alisema Adasa.

Stivo amemtaka aliyekuwa mpenziwe, Purity, kusonga mbele na maisha yake huku akimtakia neema ya Mungu katika utafutaji wa mchumba mwingine.

"Huyo mwingine, Mungu amjalie apate mwingine.. aendelee kunisapoti na aendelee na kazi yake. Ukiachana na mtu sio lazima iwe kwa ubaya," Stivo alisema.

Adasa alimshtumu Purity kwa kumshambulia baada ya video yake na Stivo wakijivinjari baharini kuonekana mitandaoni. Alimkosoa vikali kwa hilo.

View Comments