In Summary

•Yvette alifichua kuwa alikuja kugundua mahusiano mapya ya Bahati na Diana kupitia mitandao ya kijamii.

•Yvette alikiri haikuwa rahisi kwake kuweza kusonga mbele na kufichua ilimchukua miaka minne kukubali kumsamehe Bahati.

Image: INSTAGRAM

Mpenzi wa zamani wa Bahati, Yvette Obura amekiri kuwa alikumbwa na msongo wa mawazo baada yao kutengana na msanii huyo kujitosa kwenye mahusiano na Diana Marua.

Akiwa kwenye mazungumzo na Diana, Yvette alifichua kuwa alikuja kugundua mahusiano mapya ya Bahati na Diana kupitia mitandao ya kijamii.

Kwa wakati huo hakukuwa na uhusiano mzuri kati yake na Bahati na hata hawakuwa wanashirikiana katika malezi ya binti yao.

"Nilikuja kusikia kuwahusu (Diana na Bahati) kupitia mitandao ya kijamii. Mlikuwa mmepakia kuhusu Prayer Partner. Nilishangaa ni nini kinaendelea. Wakati huo mimi na Bahati hatukuwa tunazungumza. Bahati alikuwepo Mueni akizaliwa hadi ilipofika mahali tukakosana na kutengana. Tulikuwa na mizozo yetu. Huo ndio wakati mlipatana na mkawa na mambo yenu," Yvette alimwambia Diana.

Mama Mueni alisema wakati Bahati alipata kipenzi kipya yeye alikuwa anapitia mambo mengi kwa kuwa bado hakuwa ameponya jeraha la kutengana kwao na haikuwa imepita muda mrefu baada ya kujifungua.

"Niliona Baha amesonga mbele na maisha yake nikasema ni sawa. Tulikuwa na ndogo zetu. Tulikuwa wadogo hapo awali na tulikuwa na mipango ya kuwa na familia. Nilijifungua, tukatengana na akapatana na mtu mwingine.  Ikawa nashughulikia mtoto, nauguza jeraha la moyo baada ya kutengana, niko na msongo wa mawazo. Nilishangaa nifanyeje," Yvette alisimulia.

Alisema alishangazwa na jinsi mpenzi huyo wake wa zamani aliweza kujitosa kwenye mahusiano mengine haraka.

"Nilijiuliza ni msichana yupi huyo. Nilikufuatilia sana (Diana). Kila siku nilikuwa naamka naanza kuchunguza Diana Marua ni nani. Nilikuwa napitia nikagundua ni msichana ambaye alikuwa kwa video ya wimbo," Alisema.

Yvette alikiri haikuwa rahisi kwake kuweza kusonga mbele na kufichua ilimchukua miaka minne kukubali kusahau yaliyopita na kumsamehe Bahati.

Alifichua kuwa alishiriki mazungumzo na mwanamuziki huyo na hatimaye akakubali kuelewa hatua yake ya kujitosa kwenye mahusiano mengine.

Kwa sasa wapenzi hao wawili wa zamani wanashirikiana vizuri katika malezi ya binti yao Mueni. Diana pia amekuwa guzo muhimu katika maisha ya mtoto huyo.

View Comments