In Summary

•Ujumbe ulioteka umakini wa watu hata hivyo ni ule wa msanii mwenzake katika WCB Zuhura Othman almaarufu Zuchu.

•Kundi la wanamitandao walichukulia jibu la Diamond kama mzaha huku baadhi wakiamini kuwa alikuwa akionyesha wivu.

Zuchu, Mbosso na Diamond
Image: HISANI

Staa wa Bongo Mbwana Yusuf Kilungi almaarufu Mbosso ameendelea kuupigia debe wimbo wake mpya 'Huyu Hapa'.

Siku ya Jumamosi msanii huyo wa WCB alidokeza kipande cha video ijayo ya wimbo huo kupitia ukurasa wake wa Instagram.

"Huyu Haha Huyu Mmemiss Eeeh..?" aliandika chini ya video hiyo fupi.

Mamia ya wanamitandao wakiwemo watu maarufu walijumuika chini ya chapisho la Mbosso ili kuonyesha sapoti kwake.

Ujumbe ulioteka umakini wa watu hata hivyo ni ule wa msanii mwenzake katika WCB Zuhura Othman almaarufu Zuchu.

"Huyu apa huyu nampendaaa🔥🔥" aliandika.

Mmoja wa waliokuwa wepesi kujibu ujumbe wake si mwingine bali ni bosi wake na ambaye pia anadaiwa kuwa mpenzi wake, Diamond Platnumz.

Kwa utani Diamond aliuliza, "Yuko wapi?🤔"

Kundi la wanamitandao walichukulia jibu la Diamond kama mzaha huku baadhi wakiamini kuwa alikuwa akionyesha wivu.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya bosi huyo wa WCB kutupilia mbali uwezekano wa ndoa yake na Zuchu na kuhibitisha kuwa uhusiano wao wa kikazi tu bali sio wa kimapenzi kama jinsi wengi wamekuwa wakidhani.

Diamond alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya mmoja wa mameneja wake , Hamisi Shaban Taletale almaarufu Babu Tale, kumpa shinikizo kubwa  la kumuoa binti huyo wa gwiji wa muziki wa taarab ,Khadija Kopa.

"Fanya basi uoe unanichelewesha ujue," Tale alimwambia bosi huyo wa WCB chini ya video aliyopakia kwenye Instagram ikimuonyesha Zuchu akimkabidhi mkufu ghali wa dhahabu kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.

Diamond ambaye alionekana kutofurahishwa na ujumbe huo wa meneja wake alihoji jinsi angeweza kumuoa msanii wake.

"Sasa nitamuoaje wakati ni msanii wangu Boss?" alihoji. 

Katika jibu lake, pia alifafanua kuhusu busu  aliloonekana akimpa Zuchu kwenye video hiyo ambayo amefuta tayari.

"Hilo busu hapo lisiwatishe viongozi.. ni Salaam za Kijerumani hizo," alisema.

Jumatano wiki jana, Diamond alionyesha mkufu wa thamani ambao alipewa na Zuchu kama zawadi ya siku ya kuzaliwa.

Chini ya video hiyo, Diamond alimshukuru msanii huyo wake kwa zawadi hiyo na kueleza jinsi anavyomthamini.

"Maneno hayawezi kuelezea shukran yangu kwa hili Zuuh.. nisije nikatereza kuandika waandishi wakapa kutoa stori bure, ila jua nakushukuru sana, na siku zote utaendelea kuwa pale," aliandika mwimbaji huyo.

Katika video hiyo fupi, mastaa hao wawili wa Bongo walionekana wakikumbatiana kwa furaha na hata kwa wakati mmoja kubusu midomoni.

Kabla ya kufutwa, wanamitandao walijumuika chini ya chapisho hilo na kuandika maoni mseto kutokana na maudhui ya video hiyo.

Image: HISANI
View Comments