In Summary

•Mwimbaji huyo alichapisha mistari kadhaa kutoka kwa wimbo wa Lava Lava 'Inatosha' ambao unazungumzia raha za maisha bila mpenzi.

•Mapema mwezi huu 'mchumba wake' Jenny Wangui alithibitisha kuwa hawachumbiani.

Image: INSTAGRAM// STIVO SIMPLE BOY

Msanii maarufu kutoka Kibra Stivo Simple Boy amedokeza kwamba kwa sasa hayupo kwenye mahusiano yoyote na anafurahia maisha ya kuwa single!

Siku ya Jumatatu mwimbaji huyo alichapisha mistari kadhaa kutoka kwa wimbo wa Lava Lava 'Inatosha' ambao unazungumzia raha za maisha bila mpenzi.

Pia aliongeza maneno yake mwenyewe ili kueleza hali yake ya sasa katika chapisho hilo lake la Instagram.

"Mapenzi ya siku hizi jamani, sasa niko single naenjoy😂,

Jamani kuwa single raha, Akinipenda mama na baba inatosha,

Lakini ata mnivunje roho na mbavu, nikipata mwingine napenda tena❤," ulisomeka ujumbe kwenye chapisho la Simple Boy.

"Vichuna jamani!" msanii huyo alilalamika.

Haya yanajiri takriban wiki mbili baada ya mwanadada aliyedaiwa kuwa mchumba wake kukiri kwamba matendo yao ya mtandaoni pamoja ikiwemo video iliyoonyesha akivishwa pete ya uchumba na msanii huyo, yote yalikuwa kwa ajili ya kiki.

Ingawa tayari kulikuwa na hisia kwamba ni kiki, wengine walitaka kuamini kwamba mwimbaji huyo wa Kibera hatimaye alikuwa amepata mapenzi ya kweli.

Lakini mapema mwezi huu 'mchumba wake' Jenny Wangui alithibitisha kuwa hawachumbiani.

Katika video ya moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii, Wangui alisema 'uhusiano' wao umekamilika na kwamba matukio yote kwenye wa mtandaoni yalikuwa yamepangwa il kuwavutia mashabiki katika maandalizi ya mradi wa muziki.

"Ilikuwa showbiz tu, ilikua tuu biashara kusema kweli."

Alipoulizwa kama yameisha, Jenny alishika nywele zake na kuongeza "sijui, ile kitu naweza waambia, ilikuwa showbiz kama uko industry utaelewa.”

Jenny aliongeza, "Sina mahusiano, nipo single kusema kweli kwa hivyo muache kuniekea hivi na hivi."

Siku kadhaa kabla, Stivo alikuwa amefuta picha za kipusa huyo kutoka kwa kurasa zake za mitandao ya kijamii, na kuchapisha jumbe zilizoashiria kuvunjwa moyo.

Mapema mwezi huu, aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, mwanavlogu Pritty Vishy alidokeza kuwa bado ana hisia za kimapenzi kwa msanii huyo.

Katika mahojiano, Vishy aliweka wazi kuwa tangu awali alikuwa akijua kuwa Simple Boy na Gee hawangeenda mbali, iwe walikuwa pamoja kimapenzi au kibiashara alikuwa na uhakika mia kwa mia kwamba hawangedumu.

Vishy kwa mikogo ya tausi alidai hakuna mtu ambaye anaweza kumfanyia Stivo  kile ambacho yeye alikuwa anamfanyia na kusema kwamba daima pengo lake katika maisha ya mpenzi huyo wake wa zamani litabaki kuwa wazi kwani bado hapajatokea mtu na hapatawahi tokea mtu wa kuliziba.

Mimi nafasi yangu haiwezi kuzibwa kabisa, hakuna mtu anayeweza kufanya kile ambacho nilikuwa nafanya kwa Stevo Simple Boy,” alisema kwa madaha.

Aidha alipoulizwa kama huenda hivi karibuni jamii ya wanamitandao wakawaona pamoja, Pritty Vishy alidokeza kuwa huenda hivi karibuni wakawa pamoja tena kwa kuwatania watu kwamba wawe wapole na kusubiri.

“Ninyi tulieni tu, ngoja mtaona maneno, wekeni bando la kutosha kwenye simu zenu msiwe na wasiwasi,” Vishy alisema.

View Comments