In Summary

•Tricky alidokeza kuwa tatizo kubwa linalowakabili wanamuziki wa Kenya na wa Tanzania ni kikwazo cha lugha.

•Alisema suala la kizuizi cha lugha linapaswa kushughulikiwa haraka sana ili kusukuma muziki wetu mbali zaidi.

Image: INSTAGRAM// DIAMOND PLATNUMZ

Mchekeshaji Francis Munyao almaarufu MCA Tricky amebainisha kuwa si rahisi kwa wasanii wa Afrika Mashariki kufika kimataifa katika mazingira ya sasa.

Katika mahojiano na Mpasho, Tricky alidokeza kuwa tatizo kubwa linalowakabili wanamuziki wa Kenya na wa Tanzania ni kikwazo cha lugha.

Alisema lugha ya Kiswahili ambayo hutumiwa sana na wasanii wa nchi hizo mbili za Afrika Mashariki imewazuia kufikia viwango vya kimataifa.

"Wale wasanii tuko nao hapa Kenya wana talanta kubwa hata kuliko Wanigeria hawa wanafurika hapa. Chanzo kikuu cha tatizo ni kikwazo  cha lugha. Kwa nini Wanigeria hawachezi ngoma za Otile Brown, ni kwa sababu 80% ya ngoma zake ni Kiswahili. Hawaelewi Kiswahili watacheza vipi ngoma za Otile Brown," alisema.

Mchekeshaji huyo pia alidokeza kuwa Diamond Platnumz licha ya kipaji chake na jina kubwa alilonalo katika ukanda wa Afrika Mashariki ameshindwa kufika viwango vya juu kwa sababu ya kikwazo cha lugha.

"Ni kwa nini Diamond hawezi kufika viwango vya kina Burna Boy? Ni kwa sababu 80% ya nyimbo zake ni Kiswahili. Watu wanafurahia midundo tu lakini wanang'ang'ana kusikia. Kikwazo cha lugha ni tatizo kubwa," alisema.

Alisema suala la kizuizi cha lugha linapaswa kushughulikiwa haraka sana ili kusukuma muziki wa Afrika Mashariki kuenda mbali zaidi.

"Wacha tukuze utamaduni wa kuungana na ulimwengu kwa haraka kwa kujifundisha Kiingereza au Kichina," alisema.

Aidha, mchekeshaji huyo alipongeza juhudi za mchekeshaji mwenzake Eric Omondi kusukuma muziki wa Kenya kuchezwa zaidi.

Hata hivyo alibainisha kuwa wazo la Eric, licha ya kuwa nzuri,jinsi ya kulitekeleza haijafikiriwa vizuri na mengi yanaweza kufanywa kulifanikisha hilo.

View Comments