In Summary

•Stivo alikuwa akitoa hotuba kwenye mazishi hayo ya Jumamosi wakati alipomtambulisha mwenzi wake wa maisha, Grace Atieno.

•Vishy alibainisha kuwa ni sharti hafla ya harusi ifanyike ili mwanamke kutambuliwa kama mke wa mtu.

Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Image: SCREENGRAB// MUNGAI EVE

Mpenzi wa zamani wa mwimbaji Stivo Simple, Boy Pritty Vishy ameonyesha kwamba haamini  mwimbaji huyo yuko kwenye ndoa halisi na mwanamke aliyemtambulisha kama mke wake wakati wa mazishi ya marehemu baba yake.

Stivo alikuwa akitoa hotuba kwenye mazishi hayo ya Jumamosi wakati alipomtambulisha mwenzi wake wa maisha, Grace Atieno.

"Bwana asifiwe. Kwa majina mimi ni Stephen Otieno. Mimi ndiye kitinda mimba wa Anthony Adera, na huyu ndiye mke wangu," alisema mwimbaji huyo kabla ya kumpa kipaza sauti mke wake mrembo aliyesimama kando yake.

Baada ya kupokea kipaza sauti, Bi Atieno alimwomboleza baba mkwewe huku akionyesha wazi wazi ukaribu uliokuwepo kati yake na marehemu.

"Bwana asifiwe. Kwa majina ni Grace Atieno. Nimeoleka kwa Bwana Stephen Otieno. Naskia vibaya kumpoteza mtu mwenye alikuwa akinitoa kila wakati..." Grace alisema kabla ya kuzidiwa na hisia na kuangua kilio.

Vishy sasa amekicheka  kitendo cha mpenzi huyo wake wa zamani kumtambulisha mwanamke mwingine kama mke wake.

Akizungumza kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram, kipusa huyo mwenye umri wa miaka 21 alibainisha kuwa ni sharti hafla ya harusi ifanyike ili mwanamke kutambuliwa kama mke wa mtu.

"Mimi ndoa najua ni lazima kukuwe na harusi. Kama si hivyo hiyo ni 'kuja tukae' na hiyo sio ndoa," alisema.

Vishy alikuwa akimjibu shabiki aliyetaka kujua jibu lake kufuatia hatua ya Stivo kumtambulisha mke wake.

Wakati huo huo, pia aliweka wazi kuwa kuolewa haijawahi kuwa katika orodha ya matakwa yake maishani.

Siku za hivi majuzi, Vishy amekuwa akiweka wazi kwamba anaendelea kumtafuta mpenzi mpya wa kumridhi mwimbaji Stivo Simple Boy baada ya mahusiano yao kusambaratika mapema mwaka jana.

Mwezi uliopita, kidosho huyo alifutilia mbali uwezekano wa yeye kurudiana na mwimbaji huyo kutoka Kibra.

Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye mtandao wa Instagram,  Vishy aliweka wazi kuwa hana nia ya kurudiana na mpenzi wake yeyote wa zamani.

Alisema tayari amesonga mbele na maisha yake baada ya kutengana na Simple Boy na akabainisha kuwa hayupo tayari kumpa msanii huyo nafasi nyingine.

"Unaweza kumpa Stivo nafasi nyingine?" shabiki mmoja aliuliza.

Vishy alijibu, "Hapanaaa, nimesonga mbele siwezi adi."

View Comments