In Summary

•Mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa yeye na mpenzi wake mzungu watafunga pingu za maisha mwezi ujao.

•Mwanamuziki huyo alidokeza kuwa hakufanikiwa kupata gauni ambalo mpenziwe anataka humu nchini Kenya.

PICHA 1: Harusi ya kwanza ya Akothee PICHA 2: Akothee na mpenzi wake Omosh
Image: HISANI

Mwimbaji Akothee yuko njiani kuelekea jiji la Paris, nchini Ufaransa kununua gauni la harusi huku siku yake kuu ikikaribia kwa kasi.

Siku ya Ijumaa, mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa yeye na mpenzi wake mzungu watafunga pingu za maisha mwezi ujao.

"Siwezi @misteromosh .. Ni April 10," Akothee ambaye alionekana kuzidiwa na hisia ya furaha alisema kwenye Instagram.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 aliambatanisha tangazo hilo na video za bustani nzuri ambapo alidokeza kuwa harusi yake na Bwana Omosh itafanyika. Alikuwa ameenda kukagua matayarisho yanavyoendelea.

"Katika ukaguzi wa eneo la siku ya harusi yangu, mume wangu aliagiza bwawa la maji," Akothee aliandika.

Baadaye siku hiyo, alifichua kuwa anaelekea nchini Ufaransa kwa minajili ya kununua gauni linalokidhi viwango ambavyo mchumba wake anataka.

"Ninaenda katika jiji la mapenzi kwa gauni langu la harusi. Kwa hivyo unamaanisha hakuna gauni nchini Kenya," alisema kupitia Instagram.

Mwanamuziki huyo alidokeza kuwa hakufanikiwa kupata gauni ambayo mpenziwe anataka humu nchini Kenya.

Bw Schwiezer almaarufu Bw Omosh alimvisha Akothee pete ya uchumba katikati mwa mwaka jana, miezi michache tu baada ya mahusiano yao kujulikana wazi. Mwanamuziki huyo alijitosa kwenye mahusiano na Bw Omosh baada ya kutengana na aliyekuwa meneja wake, Nelly Oaks mwishoni mwa mwaka 2021.

Septemba mwaka jana, mama huyo wa watoto watano alibainisha kuwa baada ya kuhangaika miaka mingi akitafuta mapenzi, hatimaye amefanikiwa kumpata mwenzi wa maisha na yuko tayari kutulia kwenye ndoa.

Akoythee aliweka wazi kuwa yuko tayari kuwa mke kwani alihisi kama kwamba maisha yake sasa yamekamilika.

"Sikujua kijiji changu kingeweza kuwa Paradiso. Mfalme alikuwa akikosekana. Sasa naweza kusema maisha yangu yamekamilika na niko tayari kutulia, niko tayari kuwa mke mtiifu," Akothee alisema.

Siku za hapo awali, mwanamuziki huyo aliwahi kufichua kwamba harusi yake ya kwanza na aliyekuwa mumewe, Jared Okello iligharimu shilingi 2,500 tu.

Oktoba mwaka jana, alichapisha picha iliyomuonyesha na familia yake mnamo siku ya harusi iliyofanyika miongo miwili iliyopita.

"Harusi yetu iliyogharimu Sh2500 (Imara) Wanandoa wapya waliofunga ndoa wakionyesha malengo ya wanandoa katika kanisa la Awendo SDA mnamo tarehe 6 Julai, 2002," alisema chini ya picha hizo.

Aidha, alithibitisha kuwa ndoa yake na baba huyo ya binti zake watatu ilivunjwa rasmi mnamo Mei  22, 2011 baada ya kesi ya talaka kuwasilishwa mwaka wa 2007. Hi ni baada ya kuwa kwenye ndoa rasmi kwa takriban miaka mitano

View Comments