In Summary

•Kuwa wapenzi wa zamani hakujawazuia mastaa hao wa Afrika Magharibi kupeana sapoti, kusherehekeana na kuonyeshana upendo.

•Wakati akimsherehekea mwanasosholaiti huyo mnamo siku yake ya kuzaliwa, Grand P alimtaja kama mwanamke mrembo zaidi na furaha yake.

Grand P na aliyekuwa mpenzi wake Eudoxie Yao
Image: FACEBOOK// GRAND P

Sasa ni wazi kwamba hakuna uhasama wowote kati ya wapenzi wa zamani mashuhuri Moussa Sandiana Kaba almaarufu Grand P na mwanasosholaiti Eudoxie Yao licha ya kutengana miezi kadhaa iliyopita.

Mastaa hao wa Afrika Magharibi wenye tofauti kubwa za kimaumbile walikuwa kwenye uhusiano ya kimapenzi kwa takriban miaka mitatu kabla ya kuripotiwa kutengana kwa njia isiyoeleweka mwishoni mwa mwaka jana.

Hata hivyo, kuwa wapenzi wa zamani hakujawazuia wawili hao kupeana sapoti, kusherehekeana na kuonyeshana upendo.

Siku chache tu baada ya Grand P kumsherehekea Bi Eudoxie Yao mnamo siku yake ya kuzaliwa, mwanasosholaiti huyo wa Ivory Coast  sasa amesaidia kuupigia debe wimbo wake  mpya kwenye mitandao ya kijamii. Jumapili, Yao alitengeneza video ya Tiktok akicheza wimbo mpya wa mpenzi huyo wake wa zamani akimshirikisha Azaya, jambo ambalo lilimfurahisha mwimbaji huyo mwenye maumbile ya kipekee.

“Shukran Azaya, Grand P wakimshirisha Eudoxie Yao,” Grand P aliandika kwenye video ya mrembo huyo wa Ivory Coast.

Huku akimjibu, Eudoxie Yao kwa utani alisema, "Umeamka tarari? Wewe  una haraka."

Wakati akimsherehekea mwanasosholaiti huyo mnamo siku yake ya kuzaliwa, Grand P alimtaja kama mwanamke mrembo zaidi na furaha yake.

"Kheri ya siku ya kuzaliwa kwa mwanamke mrembo zaidi, furaha yangu . Nakutakia furaha yote duniani," Grand P alimwambia Bi Yao.

Mwanamuziki huyo tajiri alimtaka mpenzi huyo wake wa zamani ajiburudishe na kufurahia siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake.

Bi Yao hata hivyo alionekana kushangazwa na ujumbe wa mwimbaji huyo na kumuuliza kwa nini alimkumbuka tu siku hiyo.

"Je, ni sasa tu ambapo umenikumbuka?" alijibu.

Wapenzi hao wawili wa zamani sasa wametengana kwa miezi kadhaa.

Wiki chache zilizopita, Grand P alidokeza kuwa tayari ameshasonga mbele na maisha yake na sasa anachumbiana na mwanamke mwenye asili ya Kiasia.

Mwanamuziki huyo wa Guinea mwenye maumbile ya kipekee alimtambulisha mpenzi wake mpya, Yubai Zhang mwezi Machi na wawili hao walionekana wakijivanjari pamoja na kuonyesha muungano wao mzuri.

Wawili hao walikuwa wakisafiri katika nchi tofauti pamoja na hawakuona haya kukiri mapenzi yao mazito licha ya tofauti zao.

View Comments