In Summary

•"Siku zote ujue kwamba wewe ndio sababu ya mimi kupambana usiku na mchana ili kuhakikisha unapata furaha ambayo uliikosa kwa muda mrefu," Diamond

•Diamond aliweka wazi kuwa anampenda na kumheshimu mama yake kutokana na  juhudi zote alizowekeza ili kuweka chakula mezani.

Diamond Platnumz amemsherehea mamake na kumpuuza baby mama wake Tanasha Donna
Image: INSTAGRAM

Hivi leo, Julai 7, wanawake wawili maalum katika maisha ya mwimbaji Diamond Platnumz, mama yake Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote na mzazi mwenzake Tanasha Donna wanasherehekea siku zao za kuzaliwa.

Staa huyo wa Bongo ametumia ukurasa wake wa Instagram kueleza mapenzi yake yasiyoisha na kumsherehekea mzazi wake huyo katika siku yake hii maalum. Hata hivyo bado hakuwa amemsherehekea mama wa mtoto wake wa tatu, Naseeb Junior kufikia wakati wa kuchapishwa kwa taarifa hii.

Wakati akisherehekea Mama Dangote siku ya Ijumaa, Diamond Platnumz alitumia fursa hiyo kufufua kumbukumbu ya jinsi mzazi huyo wake  alivyopigana kusaidia familia yao wakati alipokuwa bado mdogo.

"Nakumbuka mwaka mmoja wakatio unaanza Saloon Kariakoo, tukiwa tunarudi usiku majira kama ya saa sita hivi kwenye daladala nikakwambia "usijali mama kuna siku nitatoboa kwenye muziki na nitakufungulia na wewe Saloon yako"," Diamond alisimulia.

Aliongeza, "Vyote naweza visahau lakini maneno haya siwezi yasahau, kwa sababu nilikuambia kwa uchungu, kwa jinsi nilivyokua nahangaika na maumivu ya kiti cha moto kwenye daladala ya Hiace."

Bosi huyo wa WCB aliweka wazi kuwa anampenda na kumheshimu mama yake kutokana na  juhudi zote alizowekeza ili kuweka chakula mezani.

"Siku zote ujue kwamba wewe ndio sababu ya mimi kupambana usiku na mchana ili kuhakikisha unapata furaha ambayo uliikosa kwa muda mrefu," Diamond alimwambia mamake.

Aliongeza, "Happy Birthday Mom, mwenyezi Mungu akupe Maisha marefu yenye furaha, afya na Amani @mama_dangote."

Msanii wa WCB, Zuchu, ambaye kwa muda mrefu amedaiwa kuwa kwenye mahusiano na bosi wa lebo hiyo ni miongoni mwa masta wengine ambao walimsherehekea Mama Dangote katika siku hiyo maalum kwake.

Katika ujumbe wake, binti huyo wa Khadija Kopa alimuonyesha upendo mzazi huyo wa bosi wake na kumtakia maisha marefu.

"Kheri ya siku ya kuzaliwa boss de la boss @mama_dangote Allah akupe afya na furaha Mama," Zuchu aliandika.

View Comments