In Summary

• Samidoh alidokeza aliona kitu cha kutilia shaka na kumtaka mama huyo watoto wake wawili aonyeshe upande wenye pazia.

•Karen aliomuonya rafiki huyo dhidi ya madai kuwa amemuona mwanamume chumbani na akaeleza kuwa Samidoh hapendi utani wa aina hiyo.

Samidoh na Karen Nyamu
Image: HISANI

Siku ya Jumatano usiku, seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu na mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh walishiriki katika kipindi cha moja kwa moja kwenye mtandao wa Tiktok.

Wapenzi hao pia walijumuika na rafiki zao wawili waliofahamika kwa jina la Kelvin Shaban na Wambui ambao walishiriki gumzo nao. Katika kipindi hicho, seneta Nyamu alionekana kitandani huku akiwa amevalia mavazi mepesi.

Wanne hao walipokuwa wakiendelea kupiga gumzo moja kwa moja, Karen alionyesha kuzunguka chumba chake cha kulala ikiwa ni pamoja na mahali alipokuwa ameweka picha yake na ya Samidoh. Hapo ndipo rafiki yao Shaban alipodai kuwa amemwona mwanaume anayefanana na Dedan Kimathi.

Wakati huohuo, Samidoh alionekana kudokeza kuwa pia yeye alikuwa ameona kitu cha kutilia shaka na kumtaka mama huyo watoto wake wawili aonyeshe upande wenye pazia, jambo ambalo lilimuacha na mshtuko mkubwa usoni.

“Nani huyo ako kwa taa,” Samidoh alisikika akimuuliza mzazi huyo mwenzake baada ya kuonyesha tena ndani ya chumba kutumia kamera.

Seneta huyo wa chama cha UDA alionekana kushtuka sana baada ya mpenzi wake Samidoh kudai aliona mwanaume karibu na taa na katika majibu yake alimtambua hadharani kama mpenzi wake.

“Kwa taa gani babe?” Karen Nyamu alihoji kwa mshangao.

Shaban alimuunga mkono mwimbaji huyo Mugithi akisisitiza kuwa pia yeye alimwona mwanaume ndani ya chumba cha Karen.

Kufuatia hilo, Karen alionekana kumwonya vikali rafiki huyo dhidi ya madai kuwa amemuona mwanamume chumbani na akaeleza kuwa mpenzi wake Samidoh hapendi utani wa aina hiyo.

“Wewe Shaban unajua Sam hapendi mzaha. Wee, ebu acha mzaha, unajua Sam hapendi vichekesho,” Nyamu alimbainishia Shaban.

Rafiki huyo hata hivyo aliendelea kusisitiza kuwa alikuwa amemuona mwanaume na kuhoji kwanini anafichwa.

“Anafichwa kwa nini si akuje tuongee?” aliuliza Shaban.

Baada ya wote kuonekana kuridhika kuwa hakuna mtu katika chumba cha seneta huyo wa kuteuliwa waliendelea na mazungumzo yao ambayo kwa ujumla yalikuwa ya kuburudisha na kuchekesha.

Katika wiki za hivi majuzi, seneta Nyamu na mzazi huyo mwenzake wamekuwa wakitumia muda mwingi pamoja huku mke wa Samidoh, Edday Nderitu akifurahia likizo na familia yake nchini Marekani ambako alihamia zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

View Comments