In Summary

•Seneta Nyamu alieleza imani yake kuwa siku moja atakuwa na uhusiano mzuri wa karibu na bi Edday Nderitu na kufichua kuwa huwa anaomba sana hilo litokee.

•Alifichua kuwa Edday bado anawasiliana na Samidoh na kwamba hawezi kwenda popote kwani muungano wao hauwezi kuvunjika kwa urahisi.

Edday Nderitu, Samidoh, Karen Nyamu
Image: HISANI

Seneta mashuhuri wa kuteuliwa Karen Njeri Nyamu amefunguka kuhusu hamu yake kubwa ya kutaka bi Edday Nderitu awe rafiki yake.

Katika mahojiano na na Ala C kwenye kipindi cha Reke Ciume na Ene, mama huyo wa watoto watatu alieleza imani yake kubwa kuwa siku moja atakuwa na uhusiano mzuri wa karibu na mke huyo wa mzazi mwenzake Samidoh na kufichua kuwa huwa anaomba sana hilo litokee.

Seneta Nyamu alidai kuwa yeye ni mtu mwenye upendo sana kwa kila mtu ambaye hana maringo.

“Ningependa kukumbukwa kama mtu jasiri, asiye na unafiki, asiye na kiburi, mtu anayependa watu. Huwa natamani mke mwenzangu (Edday) angekuwa rafiki yangu, hajui lakini mimi huomba kila mara, Mungu atafanya hivyo,” Karen alisema.

Seneta huyo wa UDA alidokeza kuwa hajawahi kupigana na Bi Edday wala kujibizana naye licha ya kudaiwa kumshambulia.

"Utakayosikia nikizungumza kumhusu ni mambo mazuri," alisema.

Wakili huyo alidokeza kuwa kila kitu kiko sawa katika boma la Muchoki na kwamba familia bado iko sawa licha ya tetesi kuwa ndoa ya mwimbaji huyo wa Mugithi na Bi Edday Nderitu ya zaidi ya mwongo mmoja imevunjika.

Alifichua kuwa Edday ambaye kwa sasa anafurahia wakati na familia yake nchini Marekani bado anawasiliana na Samidoh na kwamba hawezi kwenda popote kwani muungano wao hauwezi kuvunjika kwa urahisi.

“Mambo mnayoyaona kwenye mitandao ya kijamii mtashangaa sana, kuna baadhi ya miungano imetoka mbali sana. Labda hajui kwamba haendi popote, lakini najua kwa sababu miungano mingine si rahisi kukatika,” alisema.

Alidokeza kuwa mpenzi wake Samidoh na mkewe wamechukua mapumziko lakini bado wako katika uhusiano mzuri.

“Huwa naskia wakiongea, wako sawa sio vile mnafikiria. Hata watoto wanaongea naye kupitia simu yake. Kwa ground hakutawahi haribika,” alisema.

Nyamu alisisitiza kuwa yeye si mharibifu na akadokeza kuwa kuna mambo makubwa yatajidhihirisha katika siku zijazo.

View Comments