In Summary

•Katika mkutano huo, Mambo Mbotela alifichua kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Radio Jambo na vipindi vyake vizuri.

•“Muendelee hivyo hivyo, sisi twaipenda na kutumai kwamba kutakuwa na vipindi vingine vizuri vizuri vitakuja,” Mambo Mbotela alisema.

Mwanahabari mkongwe Leonard Mambo Mbotela na Gidi
Image: GIDI OGIDI

Watangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost Asubuhi, Joseph Ogidi almaarufu Gidi na mwenzake Jacob Ghost Mulee walikutana na mwanahabari mkongwe Leornand Mambo Mbotela na kushiriki naye mazungumzo ya wazi.

Gidi alishiriki baadhi ya nyakati nzuri walizokuwa nazo na gwiji huyo wa utangazaji kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Katika mkutano huo, Mambo Mbotela alifichua kuwa yeye ni shabiki mkubwa wa Radio Jambo na vipindi vyake vizuri.

“Mimi nakiliza sana Radio Jambo. Nakiliza zaidi zaidi, baadhi ya mazungumzo yenu na ucheshi wenu. Lakini kuna kipindi ambacho chaitwa Patanisho, mimi huwa sisiki kabisa. Ikifika saa mbili na nusu, niko na nyinyi. Ile mkianza tu, niko na nyinyi,” Mambo Mbotela aliwaambia Gidi na Ghost.

Aliongeza, “Kuna zingine huwa zinanichekesha sana, zingine zinanishangaza, zingine zinamchekesha hata Ghost.

Mtangazaji huyo wa zamani wa runinga ya KBC alibainisha kuwa Radio Jambo ni mojawapo ya vituo vya redio vinazopendwa na kusikilizwa sana nchini Kenya.

“Muendelee hivyo hivyo, sisi twaipenda na kutumai kwamba kutakuwa na vipindi vingine vizuri vizuri vitakuja,” alisema.

Mambo Mbotela pia aliwapongeza watangazaji Gidi na Ghost kwa kazi yao nzuri na kuwashukuru kwa kuwajengea asubuhi mamilioni ya Wakenya ambao hufuatilia kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi.

Wakati huohuo, Gidi alifunguka kwamba katika taaluma yake ya utangazaji kwa zaidi ya miaka 16, siku zote amekuwa akitamani kama kungekuwa na uwezo wa kurudisha muda nyuma na apewe nafasi ya kuchagua mtangazaji wa kufanya kazi naye basi angemchagua mtangazaji huyo mkongwe  wa VOK.

Gidi alisema kwamba angefurahi sana kufanya kazi naye ingekuwa ni uwezo wa kurudisha muda nyuma angalau kidogo tu.

“Nimefanya utangazaji wa redio kwa miaka 16, lakini ikiwa ningepewa nafasi ya kushikanishwa na mtu wa redio, nitamchagua gwiji Leonard Mambo Mbotela,” Gidi alisema.

Hata hivyo, Gidi hakumpuuza mtangazaji mwenza Ghost Mulee ambaye wamekuwa wakifanya kazi naye kwa miaka kadhaa kwenye Radio Jambo awamu ya Asubuhi na kusema kwamba wangeungana na Mbotela ingekuwa ni timu moja hatari sana ya kuteka mawimbi ya utangazaji nchini.

“Hebu fikiria Mbotela, Gidi na Ghost Asubuhi? Vicheko baada ya vicheko…Tunasherehekea kwa fahari lejendari Leonard Mambo Mbotela,” aliongeza.

Mambo Mbotela kwa sasa amestaafu baada ya kufanya kazi katika shirika la habari la serikali ya Kenya, KBC kwa Zaidi ya miongo minne.

View Comments