In Summary

•Bi Amina Khalef sasa ameweka wazi kwamba madai hayo ni ya kipuuzi, ni ya nia mbaya na ni ya kushangaza.

•Amina amelaani kitendo cha kuhusishwa bila hatia katika vita vya maneno vinavyoendelea kati ya mastaa hao wawili wa bongo.

Alikiba, Amina Khalef, Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM//

Mke wa mwimbaji Alikiba, Amina Khalef hatimaye amejibu baada ya kuingizwa kwenye mgogoro unaodaiwa kuwepo kati ya baba huyo wa watoto wake wawili na mpinzani wake mkuu Naseeb Abdul Juma almaarufu Diamond Platnumz.

Huku akimshambulia Alikiba na kudhalilisha kazi yake ya muziki katika taarifa yake Jumapili jioni, Diamond alidai kuwa pia aliwahi kutoka kimapenzi na mke wa bosi huyo wa lebo ya King’s Music.

"Usiongee maana habari yangu hadi na Amina nadhani unayo...." Diamond Platnumz alidai siku ya Jumapili.

Haya basi, shutuma hizo nzito kwa hakika zilimfikia Bi Amina ambaye sasa ameweka wazi kuwa madai hayo ni ya kipuuzi, ni ya nia mbaya na ya kushangaza.

Amina ambaye alichukua talaka dhidi ya baba huyo wa watoto wake wawili mwaka jana alilaani kitendo cha kuhusishwa bila hatia katika vita vya maneno ambavyo vimekuwa vikiendelea mitandaoni kati ya mastaa hao wawili wa bongo fleva.

"Ni upuuzi, ni mbaya na ni jambo la kushangaza kuhusisha wanadamu wasio na hatia katika migogoro/vinyongo. NINALAANI KIWANGO CHA JUU CHA KUTOHESHIMU wanawake,” Bi Amina Khalef alisema kupitia akaunti yake ya Instagram.

Aliongeza, "Bila hisia za heshima, kuna nini cha kutofautisha wanaume na wanyama? UADILIFU WA BINADAMU HAUHUSIKI.”

Licha ya mkewe kutajwa na Diamond katika mashambulizi ya moja kwa moja kwake, Alikiba bado hajajibu kuhusu madai mazito ya mpinzani wake mkuu.

Madai ya bosi huyo wa WCB hayakuchukuliwa vyema na watumiaji wengi wa mitandao ya kijamii ambao walisema Diamond alipaswa kuzozana na Alikiba tu bila kuihusisha familia yake.

Talaka ya Alikiba na mzazi huyo mwenzake Amina Khalef kutoka Kenya iligonga vichwa vya habari mapema mwaka jana.

Ombi la talaka liliwasilishwa mahakamani na Bi Amina mwezi Februari na kusikilizwa kwa miezi kadhaa kabla ya kuamuliwa.

Miezi kadhaa baadaye, mama huyo wa watoto wawili alitangaza kuwa yupo 'huru rasmi', ujumbe ambao ulieleweka kumaanisha kesi ilikuwa imekamilika.

Amina, ambaye sio maarufu sana kwenye mitandao ya kijamii, alipakia picha ya ngome iliyo wazi na ndege akiruka.

Pia alifuta picha zote na AliKiba, zikiwemo zile za harusi yao ya kifahari iliyofanyika mnamo Aprili 2018.

View Comments