In Summary

•Rapudo aliweka wazi kuwa hajali ni nani alikuwa na mwanasosholaiti huyo mrembo kabla yake huku akibainisha kuwa anaonekana bora akiwa naye sasa.

"Nitakutunza wewe na moyo wako vizuri zaidi kuliko mtu yeyote katika siku zako zilizopita, na hiyo ni kweli," Rapudo alimwambia Amber Ray.

Amber Ray na mpenziwe Kennedy Rapudo
Image: INSTAGRAM// AMBER RAY

Mfanyabiashara Kennedy Rapudo ameendelea kuthibitisha mapenzi yake makubwa kwa mkewe na mzazi mwenzake, mwanasosholaiti Faith Makau almaarufu Amber Ray.

Katika taarifa yake siku ya Jumanne jioni, baba huyo wa watoto wawili aliweka wazi kuwa hajali ni nani alikuwa na mwanasosholaiti huyo mrembo kabla yake huku akibainisha kuwa anaonekana bora akiwa naye sasa.

"Sijali nani alikuwa na wewe kwanza na sijali ni nani alikuwa na wewe muda mrefu zaidi, kwa sababu ukweli ni kwamba, unaonekana bora ukiwa nami," Rapudo alisema.

Mfanyibiashara huyo aliendelea kumpa mkewe ahadi nzuri kwamba, "Nitakutunza wewe na moyo wako vizuri zaidi kuliko mtu yeyote katika siku zako zilizopita, na hiyo ni kweli."

Katika jibu lake, mama huyo wa watoto wawili alimshukuru mume wake Rapudo kwa kurekebisha moyo wake ambao ulivunjwa na wapenzi wa zamani.

"Asante kwa nia yako ya kurekebisha kile ambacho hukuwahi kuvunja," Amber Ray alijibu taarifa ya mumewe kwenye Instagram.

Wapenzi hao wawili wamekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa takriban mwaka mmoja sasa. Walianza kuchumbiana Mei mwaka jana, miezi michache tu baada ya Amber Ray kuachana na mfanyabiashara Jimal Rohosafi ambaye alichumbiana naye kwa takriban mwaka mmoja.

Mwezi Machi, kupitia chaneli yake ya YouTube, Amber Ray alifichua alipokutana na Rapudo na kusema hakuwahi kufikiria  wangeweza kuchumbiana.

Alidokeza kuwa wakati huo aliogopa kuingiza mapenzi pichani kwani alihisi kama kwamba ingeharibu uhusiano wao.

"Sikuwahi kuona tukiwa na kitu. Wewe ni mzuri. Nilitaka kukuweka kama rafiki na nilijua tukilala pamoja tungeharibu," Amber Ray alimwambia Rapudo.

Aliongeza kuwa wakati huo, Rapudo alionekana kama mtu asiye mwaminifu.

"Ulionekana kama mchezaji lakini umetulia sana," alisema.

Wawili hao walikutana vipi?

"Tulikutana kwenye hafla kupitia rafiki. Tukawa marafiki bila masharti yoyote kabla ya kuanza kuchumbiana," Amber Ray alisema.

Sherehe hiyo ilifanyika kando ya barabara ya Thika.

Kulingana na Amber Ray, mumewe ana majivuno na ubinafsi mkubwa na hata alishangaa wamewezaje kufikia uhusiano wao hadi sasa.

"Wewe ni mpenzi na majigambo mengi. Una kiburi cha siku na maringo. Kwa kweli, hadi hapa, ni kwa neema ya Mungu," alisema.

Rapudo kwa upande wake alimshutumu mkewe kwa kuwa mtumizi mkubwa wa pesa, na kuongeza kuwa yeye hununua vitu visivyo vya lazima.

"Unaenda kufanya manunuzi kila wakati, unanunua vitu visivyo vya lazima. Una nguo na viatu vingi," Rapudo alisema.

View Comments