In Summary

•Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 hata hivyo alikiri kuwa tayari ametamani nyumbani baada ya kuwa nje kwa zaidi ya wiki moja.

•Akothee alidokeza kuwa baadhi ya mambo nchini Kenya ikiwamo udaku na uhuru wa kelele humfanya atamani nyumbani kila anaposafiri.

Akothee na mumewe Denis Shweizer wakifurahia fungate jijini Santorini, Ugiriki.
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee kwa sasa anafurahia muda wake nchini Uswizi baada ya kufanya shoo yenye mafanikio nchini Uswidi wikendi.

Katika taarifa yake Jumatano jioni, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 hata hivyo alikiri kwamba tayari ametamani nyumbani baada ya kuwa nje kwa zaidi ya wiki moja.

Akothee aliweka picha yake akifurahia muda katika nchi hiyo ya Ulaya na kwa maelezo yake alionekana kushangaa kwa nini anajikuta akimiss Kenya.

“Aaah, nimemiss nyumbani tayari. Kwani nilirogwa na Kenya?” Akothee aliandika.

Katika taarifa nyingine, mama huyo wa watoto watano alidokeza kuwa baadhi ya mambo nchini Kenya ikiwamo udaku na uhuru wa kelele humfanya atamani nyumbani kila anaposafiri kuenda nje ya nchi, jambo linalomfanya kuwa na mawazo ya kuhama.

“Kila nikifikiria kuhama, nakumbuka jinsi nitakavyopeza udaku na kelele. Hapa unaambiwa muziki uko juu sana.. Sasa nammiss baba yangu. Naskia kwenda kutoa nguo, Senye Beach Migori county dalawa,” Alisema.

Mapema wiki hii, Akothee alizua hisia mseto kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kufuatia chaguo lake la mtindo wa mavazi wakati alipokuwa akitumbuiza mbele ya mashabiki wake jijini Stockholm, Uswidi wikendi.

Jumatatu jioni, msanii huyo alishiriki na mashabiki wake baadhi ya picha zake akitumbuiza jukwaani katika nchi hiyo ya Ulaya, ambapo alionekana akiwa amevalia vazi jeusi lenye utata lililofunika tu sehemu ya juu ya mwili wake.

Kabla hata wanamtandao hawajatoa maoni yao kuhusu picha hizo, jambo ambalo bila shaka lilitarajiwa, alitumia sehemu ya maelezo ya chapisho hilo kujitetea na kuweka wazi kuwa yeye si mfano wa kuigwa kwa mtu yeyote.

“Huyu Ndiye AKOTHEE MSANII. Mwimbaji, mburudishaji na sio aina yako ya mfano. Msanii huyu Akothee ana soko lengwa tofauti leo. Weka mdomo wako mahali pesa zako zilipo. Akiwa na Dj Ike anayetafutwa zaidi. SWEEEEEDEN ilikuwa MOTO. Asante sana. HATUA NYINGINE,” Akothee alisema chini ya picha hizo.

Pichani, alionekana akiwapa mashabiki wake shoo ya kusisimua kwa huku wanadensi wa kike wakicheza nyuma yake.

Wanamitandao waliotoa maoni kwenye chapisho hilo walionekana kuvutiwa zaidi na vazi lake jeusi lililofunika tu sehemu yake ya juu ya mwili wake. Ukaguzi wa karibu wa picha hizo hata hivyo unaonyesha kuwa miguu na mapaja yake, licha ya kuwa yalionekana, yalifunikwa na nguo nyepesi.

Baadhi ya Wakenya waliotoa maoni walionekana kutoridhishwa na vazi la mwimbaji huyo na kwa hilo wakamshambulia huku wengine wakimtetea na kubainisha kuwa pia wanariadha na masta wengine wa kimataifa huwa wanaburudisha wakiwa wamevalia mavazi yasiyofunika mwili wote na huwa hawahukumiwi.

View Comments