In Summary

•Msanii huyo mwenye umri wa miaka 41 alisisitiza kwamba hawezi kutaja idadi halisi ya watoto ambao amewapata.

•Pia funguka kuhusu tukio lililotokea akiwa kidato cha nne ambapo msichana aliyekuwa akichumbiana naye alidai kuwa na ujauzito wake

ERIC OMONDI NA MPENZIWE LYNNE NA MTOTO WAO

Mchekeshaji maarufu wa Kenya Eric Omondi amekiri wazi kuwa hana uhakika kabisa ana watoto wangapi.

Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio cha humu nchini siku ya Jumatano, Eric alitoa makadirio ya watoto wake ambao anawafahamu kuwa 3 ama 4.

Mchekeshaji huyo ambaye aligeuka kuwa mwanaharakati hata hivyo alidokeza kuwa kuna uwezekano mkubwa kuwa ana watoto wengine wengi.

“Wangu wa kibinafsi sijui nitasema ni watatu, wanne.. tuseme watatu,” Eric alijibu wakati alipoulizwa idadi kamili ya watoto wake.

Licha ya kutoa makadirio, msanii huyo mwenye umri wa miaka 41 alisisitiza kwamba hawezi kutaja idadi halisi ya watoto ambao amewapata.

Aliendelea kufunguka kuhusu tukio ambalo lilitokea akiwa katika kidato cha nne ambapo msichana mmoja ambaye alikuwa akichumbiana naye alidai kuwa na ujauzito wake, madai ambayo bado hajafanikiwa kuthibitisha hadi leo.

“Kule Kisumu kitambo nikiwa shule kuna msichana alikuja nyumbani, anaitwa Rose. Mama aliniita akaniambia kuwa kuna msichana ananiita na anasema ako na ujauzito wangu. Nilikuwa form 4. Nakumbuka hadi leo. Sijui kama ilikuwa kweli, mimi nilikuwa shuleni. Niligombanishwa, nikirudi shuleni mtoto akaja tukapoteleana mpaka leo,” alisimulia.

Mchekeshaji huyo wa zamani wa Churchill Show alikiri kwamba alifahamiana na mwanadada huyo wakati huo na akasema kuna uwezekano kwamba madai yake kuhusu yeye kumpa mimba yalikuwa ya kweli kwani walikuwa wapenzi.

Kwa muda mrefu sasa, Eric Omondi pia amekuwa akidaiwa kuwa na mtoto mvulana na mwanahabari Jackie Maribe.

Mwaka wa 2021, wasanii hao wawili ambao walidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi katika miaka ya nyuma walivuana nguo hadharani na kutupiana cheche za maneno kuhusiana na majukumu ya malezi.

Ugomvi wao ulikuwa mbaya kiasi cha Eric kufikia hatua ya kuibua shaka ya kuwa mzazi mwenza wa mtangazaji huyo wa zamani. Huku wakiendelea kujibizana, wakati mmoja alidai kwamba alishiriki tendo la ndoa na Maribe mara moja tu mnamo mwaka wa 2012 baada ya wao kubugia chupa kadhaa za mvinyo. 

"Tulipatana Radio Africa mwaka wa 2012. Nilikuwa nafanya kazi Radio Jambo na Jacque alikuwa anafanya kazi Kiss TV. Usiku mmoja baada ya sherehe na kunywa chupa kadhaa za whiskey na mvinyo Jacque na mimi ikatendeka. Ilikuwa jambo la usiku mmoja kwani alikuwa anachumbia Sam Ogina wa KTN" Omondi alisema. 

Mchekeshaji huyo asiyepungukiwa na drama alidai kwamba alihakikisha kwamba ametumia kinga wakati aliposhiriki mapenzi na Maribe.

Wawili hao baadaye walipatanishwa na mfanyibiashara Simon Kabu na hatimaye wakaomba radhi kwa Wakenya kwa waliyosema hadharani.

View Comments