In Summary

• “Na kwa kufanya hivyo, tunapata muda mzuri wa kujiandaa kukaribisha watoto wa mbuzi hawa wote" - alisema.

Mbuzi
Image: Hisani

Mkulima mmoja kwenye mtandao wa TikTok amejawa na furaha baada ya kugundua kwamba mbuzi wake 34 walishika mimba kwa wakati mmoja na kupiga tathmini kwamba wote watazaa kwa wakati mmoja pia.

Mkulima huyo alipakia video hiyo kwenye ukurasa wake wa TikTok akitoa masomo kwa wakulima wengine jinsi ya kugundua kwamba mbuzi wake wote wanataka mimba na kuwatafutia beberu.

Kulingana naye, yeye husoma mbuzi na anajua kwa usahihi wanapokuwa kwenye joto. Alisema hii inamwezesha kujua wakati wa kutambulisha mbuzi-dume.

“Je, unajua unaweza kuwapa mimba mbuzi wako wote kwa wakati mmoja? Hivi ndivyo unavyofanya,” aliandika kwenye video hiyo yenye mada “Jinsi ya kufanya mbuzi wako kushika mimba kwa wakati mmoja.”

Kwenye video hiyo alieeza mithili ya mwalimu anayeeleza wanafunzi jinsi ya kufanya hesabu vizuri ili kuhakikisha kwamba mbuzi wanaafikia muda wa kuhitaji mimba kwa wakati mmoja.

“Kuwafanya mbuzi wako wapate mimba wote kwa mara moja ni rahisi, hivi ndio tunafanya. Mbuzi hupata joto la kutaka mimba mara moja kwa kila mwezi, na tunahakikisha kwamba mwezi wa kwanza mbuzi wote wanapitisha ule muda wao wa joto bila kupata mimba, mwezi unaofuata unapoanza, tunawaleta mbuzi wote pamoja na kumuongeza beberu kule,” alianza kueleza.

“Kwa sababu wote walikosa muda wao wa joto mwezi uliopita, wote watapata joto hilo ghafla pindi wanaponusa harufu ya beberu miongoni mwao. Na kwa haraka beberu ataanza kuwapanda na kuwapa mimba.”

“Tulifanya hivyo mwezi huu kwa kuweka beberu miongoni mwa mbuzi wa kike 34 na tulifanya hivyo Septemba 1 na kufikia Septemba 15 alikuwa amewapa wote mimba. Kwa hiyo hawa mbuzi wote watazaa kwa wakati mmoja Januari mwakani. Kwa sababu mimba huwa ya miezi 5.”

“Na kwa kufanya hivyo, tunapata muda mzuri wa kujiandaa kukaribisha watoto wa mbuzi hawa wote na kila kitu ambacho kinahitajika kufanyika tutakifanya kwa wakati mmoja kuliko kila mbuzi kupata mtoto kwa wakati wake tofauti na kuzua mkanganyiko,” alimaliza.

View Comments