In Summary

•Akothee amewasihi watu kumsaidia kuripoti akaunti ya Facebook inayomuiga mume wake na kutumiwa kwa malengo maovu.

•Mwenye akaunti hiyo hakutumia tu jina la mume wa Akothee bali pia picha zao zilizopigwa mnamo siku ya harusi yao.

Image: FACEBOOK// AKOTHEE

Akothee amewasihi wanamitandao kumsaidia kuripoti akaunti ya Facebook inayomuiga mume wake Denis ‘Omosh’ Shweizer na kutumiwa kwa malengo maovu.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 mnamo siku ya Jumanne alichapisha screenshot ya akaunti hiyo yenye wafuasi zaidi ya elfu kumi na moja na kuweka wazi kwamba si ya Bw Denis Shweizer halisi.

Alidai kuwa akaunti hiyo ilikuwa ikitumiwa kulaghai watu kwa kuwataka watume pesa, kitendo ambacho kilimkera sana na akakilaani vikali.

"Akaunti hii feki sasa inatumia watu jumbe na kuwaomba watume pesa, tafadhali nisaidieni kuripoti akaunti hii. Omondi Denis hakuwahi kwenye Facebook na hayuko kwenye Facebook,” Akothee alisema.

Aliongeza, "Hii ni mbaya sana. Kuwa na utu. Ripoti akaunti hii Dennis Schweizer Omosh. Huyu jamaa hana habari yoyote. Si poa. Furahia kadri uwezavyo, lakini usiwe na ukatili huu. Nisaidieni kuripoti akaunti hii. Asanteni."

Kulingana na screenshot iliyoshirikiwa na mwanamuziki huyo, akaunti hiyo haikutumia tu jina la mumewe bali pia picha zao zilizopigwa mnamo siku ya harusi yao.

Kufikia wakati wa kuchapishwa kwa makala haya, picha za Akothee na Omosh zilikuwa zimeondolewa kwenye akaunti hiyo lakini jina ‘Dennis Schweizer Omosh’ lilikuwa halijabadilishwa.

Akaunti 'Dennis Schweizer Omosh' - kabla ya picha kutolewa.
Akaunti 'Dennis Schweizer Omosh' - baada ya picha kutolewa.

Haya yanajiri saa chache tu baada ya akaunti ya Instagram ya Bw Schweizer kuzimwa siku ya Jumatatu.

Saa chache tu baada ya mwanamuziki huyo kutoa taarifa ya kutia wasiwasi akifichua kwamba mambo hayajakuwa sawa kabisa katika maisha yake katika miezi michache iliyopita baada ya kupata ukweli fulani, akaunti ya Instagram ya mume wake yenye wafuasi zaidi ya elfu sabini ilitoweka Jumatatu.

Akaunti ya Instagram ya Mister Omosh ilizimwa siku ya Jumatatu na kuzidisha uvumi kwamba kunaweza kuwa na matatizo fulani ambayo bado hayajafichuliwa. Akaunti hiyo ilikuwa na takriban wafuasi 72,000 kabla ya kutoweka. Hata hivyo, haijulikani ikiwa akaunti imezimwa kwa muda au kabisa.

Akothee tayari alikuwa ameacha kufollow akaunti hiyo kabla haijazimwa na pia alikuwa amefuta picha kadhaa za mume huyo wake mzungu.Mama huyo wa watoto watano pia alikuwa amefanya mabadiliko kadhaa kwenye akaunti yake ya Instagram, akiondoa jina 'Mrs Omosh' kutoka kwa wasifu wake.

View Comments