In Summary

•Baba huyo wa mtoto mmoja hata hivyo alidai kwamba haijakuwa rahisi kwake kuhusika katika maisha ya bintiye.

•Mchekeshaji huyo alibainisha kuwa haelewi tatizo liko wapi kati yake na mpenziwe huyo wa zamani.

Carrol Sonnie na aliyekuwa mpenzi wake Mulamwah
Image: HISANI

Mchekeshaji mashuhuri wa Kenya David Oyando almaarufu Mulamwah ameeleza nia yake ya kusaidia katika malezi ya mtoto wake na aliyekuwa mpenzi wake, muigizaji Caroline Muthoni, maarufu kama Carrol Sonnie.

Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram, baba huyo wa mtoto mmoja hata hivyo alidai kwamba haijakuwa rahisi kwake kuhusika katika maisha ya bintiye.

Alidai kuwa kila anapotuma pesa au zawadi za kumtunza binti huyo wake wa miaka miwili, hurejeshwa kwake.

"Ninajaribu kusaidia lakini sio rahisi. Unatuma pesa zinareversiwa. Hata birthday nimetuma zawadi ikarudishwa. Hivyo inakuwa ngumu sana,” Mulamwah alimjibu shabiki aliyetaka kujua ikiwa anasaidia katika malezi ya bintiye.

Mchekeshaji huyo mwenye umri wa miaka 30 alibainisha kuwa haelewi tatizo liko wapi kati yake na mpenziwe huyo wa zamani.

Image: INSTAGRAM// MULAMWAH

Hivi majuzi, Sonnie alizidiwa na hisia baada ya kuulizwa iwapo Mulamwah anamsaidia katika malezi na matunzo ya binti yao.

Japo hakuweza kujibu moja kwa moja swali hilo, Sonnie alionekana kuegemea upande kwamba huenda Mulamwah tangu alipoweka wazi katika mitandao ya kijamii kuwa mtoto huyo si wake, hajawahi rudisha fikira nyuma na pengine huenda hatoi matunzo yoyote kwa ajili ya mwanao.

Sonie alimtaka mwanahabari Nicholas Kioko kumuuliza Mulamwah swali hilo kwani yeye ndiye yuko katika nafasi nzuri ya kujibu iwapo anasaidia katika malezi au la.

“Aaah, kusema ukweli hizo stori huwa sitaki kuongelea sana unajua tushatoka huko. Cha umuhimu sasa hivi ni kwamba Keilah ako vizuri, anakua. Lakini pia nahisi mtu huyo uliyemtaja [Mulamwah] anafaa kuulizwa swali sahihi, swali kama [Sonie alicheka] … sote tunajua kwamba alimkataa mwanawe. Sijui mbona hammuulizi swali hilo kwamba ni kweli ulikataa mwanao,” Carrol Sonie alijibu kwa kujikaza.

Muigizaji huyo alisisitiza mambo huenda yakawa sawa kama kweli Mulamwah ataulizwa maswali sahihi kuhusu makuzi ya binti yake Keilah.

“Inafaa mmuulize maswali kama ‘Keilah ni mwanao, ndio ama hapana’” Sonnie alitoa mwongozo wa maswali kwa wanahabari.

Mulamwah na Carrol Sonnie walitengana mwishoni mwa mwaka 2021, miezi michache tu baada ya binti yao, Keilah Oyando kuzaliwa.

View Comments