In Summary

•Muigizaji Carrol Sonnie amethibitisha kuwa anaendelea vyema baada ya kunusurika kwenye ajali mbaya ya barabarani.

•Sonnie alionyesha akitembea vizuri na haraka, akicheka, akinengua kiuno na kuinua mikono kuthibitisha kuwa yuko sawa.

Image: HISANI

Muigizaji na mtayarishaji wa maudhui maarufu wa Kenya Caroline Muthoni Ngethe almaarufu Carrol Sonnie amethibitisha kuwa anaendelea vyema baada ya kunusurika kwenye ajali mbaya ya barabarani.

Siku ya Alhamisi jioni, mpenzi huyo wa zamani wa mchekeshaji David Oyando almaarufu Mulamwah alifichua kuwa alikuwa na bahati ya kuwa hai kwani alihusika katika ajali ya barabarani mapema siku hiyo.

Katika taarifa fupi kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, mama huyo wa binti mmoja alibainisha kuwa yeye na wengine aliokuwa nao nusura wapoteze maisha yao baada ya gari walilokuwamo kupata ajali. Aidha, alifichua kuwa tukio hilo la kutisha lilimwacha akiwa na kiwewe sana.

“Aki Mungu. Karibu tupoteze maisha katika ajali ya gari.. Mungu wetu ni Mungu wa nafasi nyingine. Nimeingiwa na kiwewe sana. Woi Mungu,” Carrol Sonnie alisema kupitia Instastori zake.

Aliambatanisha taarifa yake na emoji za hisia ili kueleza jinsi tukio hilo la siku ya Alhamisi lilivyokuwa la kutisha na la kutia wasiwasi.

Katika chapisho lingine la Ijumaa jioni, muigizaji huyo mrembo hata hivyo aliondoa wasiwasi miongoni mwa mashabiki wake akifichua kuwa sasa yuko katika hali nzuri.

“Mungu ni mwaminifu. Sasa niko sawa. Asante kwa simu na jumbe zenu," alisema.

Carrol aliambatanisha ujumbe wake na video yake akitembea vizuri na haraka, akicheka, akinengua kiuno na kuinua mikono kuthibitisha kuwa yuko sawa.

Habari kuhusu ajali hiyo zilizua wasiwasi miongoni mwa mashabiki wa muigizaji huyo, ambao sasa wameeleza kufarijika kwao baada ya kujua yuko sawa.

View Comments