In Summary

•Bi Musila alisifu mapenzi mazito aliyo nayo mume wake Guardian Angel kwake huku akijigamba kuwa yanamfanya ajihisi mtoto.

•Alifichua kuwa tangu walipoamua kufanya maisha pamoja, wanatumia muda mwingi pamoja na ni mara chache huwa mbali na kila mmoja.

Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Mke wa mwimbaji wa nyimbo za Injili, Guardian Angel, Bi Esther Ngenyi Musila ameisherehekea na kuisifia ndoa yao ya miaka mitatu.

Wakati akizungumza katika mahojiano ya hivi majuzi na kituo kimoja cha habari cha Tanzania, malkia huyo mwenye umri wa miaka 53 alisifu mapenzi mazito aliyo nayo mume wake Guardian Angel kwake akijigamba kuwa yanamfanya ajihisi mtoto.

Bi Musila alisema kuwa mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 35 anampenda sana bila masharti, jambo ambalo linampa utimilifu mkubwa moyoni mwake.

“Hata bila kumwambia, yeye (Guardian Angel) anajua nampenda sana sana. Kwa sababu amenipa kutimiza maishani mwangu kupita nilivyotarajia,” Esther Musila alisema.

Aliongeza, “Kwa vile ananipenda, kwa vile ananifanyia, yaani nahisi kama mimi ndiye mtoto kwake sasa. Nimeacha kuwa mama kwa umri wangu. Yaani najiskia kama mimi ni mtoto kabisa kwa sababu ya upendo alio nao kwangu.”

Mama  huyo wa watoto watatu wakubwa alibainisha kuwa yeye na Guardian Angel wana urafiki mzuri sana na wenye nguvu ambao unawaunganisha pamoja.

Pia alifichua kuwa tangu walipoamua kufanya maisha pamoja, wanatumia muda wao mwingi pamoja na ni mara chache huwa mbali na kila mmoja.

“Yaani sisi huwa hatuachani, wakati ambao tunaachana ni labda tu nikienda kazini naye aende kazini. Lakini 99% ya maisha yetu huwa tuko pamoja,” alisema.

Aliongeza, “Ningependa tu kumwambia, yaani mpenzi nakupenda tena sana sana. Kutoka kichwani mwangu hadi kidole cha mguu.”

Mhasibu huyo mwenye umri wa miaka 53 alisema kuwa yeye na mumewe wana muungano mkubwa sana na kusema kwamba wao ni marafiki zaidi kuliko wanandoa.

“Yaani ukipata tuko wawili tu kwa nyumba, tuna utoto, utashangaa hawa ni watoto wagani. Nadhani muungano wetu ni mkubwa, sisi ni marafiki zaidi ya kuwa mume na mke. Ukiniona ninang’ara hivi, yaani ni kupendwa,” alisema.

Aidha, Bi Musila pia alibainisha kuwa katika maisha yake ya zaidi ya miaka 50, hajawahi kuwa na furaha zaidi ya aliyo nayo kwa sasa.

View Comments