In Summary

•Latifah alionekana akinyata kuelekea kwa mfanyibiashara huyo wa Uganda na kumwekelea mikono taratibu ili kuzuia kumwamsha.

•Tukio hilo ni kiashiria kingine cha uhusiano mzuri kati ya mume wa Zari, Shakib Lutaaya na watoto wake, haswa wale wawili wadogo.

Image: INSTAGRAM// SHAKIB CHAM

Ilikuwa ni kipindi kizuri  wakati binti ya mwanasosholaiti Zari Hassan, Latifah Dangote alionekana kucheza na baba yake wa kambo Shakib Cham Lutaaya akiwa usingizini.

Katika video iliyochapisjwa na Shakib kwenye ukurasa wake wa Instagram, msichana huyo mwenye umri wa miaka minane anaonekana akinyata kuelekea kwa mfanyibiashara huyo wa Uganda mwenye umri wa miaka 31 na kumwekelea mikono taratibu ili kuzuia kumwamsha.

Shakib ambaye alikuwa amejilaza kitandani bila shati alionekana kuwa na usingizi mzito na hangeweza kujua kilichokuwa kikiendelea mbele yake.

“Wakati umelala lakini Latifah ana mipango mingine..,” Shakib aliandika chini ya video hiyo.

Video hiyo ilionekana kuwa imerekodiwa na Zari mwenyewe kwani akisikika akiongea kwa nyuma.

Tukio hilo ni kiashiria kingine tu cha uhusiano mzuri kati ya mume wa Zari, Shakib Lutaaya na watoto wake, haswa wale wawili wadogo. Hii sio mara ya kwanza kwa uhusiano mzuri kati ya Shakib na Tiffah kuonekana wazi. Wawili hao wameonekana kuhusiana vizuri katika siku za nyuma.

Mapema mwaka huu, Shakib alichapisha video nzuri zake na watoto wawili wadogo wa mkewe Zari wakifurahia muda pamoja kwenye ukumbi wa mazoezi. Alionekana akiwasaidia watoto hao wa Diamond kufanya mazoezi kwa kutumia vifaa tofauti kwenye gym moja nchini Afrika Kusini ambako wanaishi.

Katika video za kwanza, mfanyibiashara huyo wa Uganda alionekana akiwainua Tiffah na Nillan hadi kufikia nguzo ambayo ilikuwa juu sana na kuwasaidia kufanya mazoezi. Baadae alionekana akiwatazama wawili hao walipokuwa wakivuta kamba nzito ya mazoezi kabla ya kuwapa mafunzo ya ndondi.

"Wakati wa kusonga," Shakib alisema chini ya video iliyomuonyesha akiwafundisha watoto hao wawili mitindo ya ndondi.

Hapo awali, Zari alikuwa ameshiriki video nzuri ya mume wake Shakib akikaribishwa nyumbani na binti yake Tiffah  kwa njia ya kupendeza sana.

Katika video hiyo ambayo Zari alichapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram, Tiffah ambaye ni mtoto wa kwanza wa mwanasosholaiti huyo na Diamond Platnumz alionekana akimkimbilia Shakib alipokuwa akishuka kwenye gari lake.  

Punde baada ya malkia huyo wa miaka minane kufika pale alipokuwa Shakib, babake huyo wa kambo alimkumbatia vizuri na kumuinua kwa mikono miwili. Wawili hao kisha walionekana kuwa na mazungumzo mafupi nje ya gari.

Zari alionekana kufurahishwa sana na uhusiano mzuri ulioonyeshwa kati ya mumewe huyo mwenye umri wa miaka 32 na bintiye. Aliambatanisha video yake na wimbo “I love you baby” wa Emilee.

View Comments