In Summary

•“Ugali kusema ukweli nakula gorogoro nne siku moja. Gorogoro nne za mahindi zisiagwe nipikiwe, nikule pamoja na sukuma besheni nne," alisema.

•Pia alidai kuwa kawaida huwa anakunywa lita thelathini za maji kwa siku.

Isaac Otesa
Image: HISANI

Jamaa mrefu kutoka kaunti ya Bungoma anayevuma mitandaoni, Isaac Otesa amefunguka kuhusu milo na vinywaji vingapi anavyotumia kwa siku.

Akizungumza katika mahojiano ya hivi majuzi,  jamaa huyo ambaye alipata umaarufu mapema mwezi huu kufuatia kulinganishwa na kijana Bradley Marongo almaarufu Gen-z Goliath, alifichua kwamba yeye hula sana kwa siku moja.

Alibainisha kuwa mwili wake hutumia nguvu nyingi, na kumfanya awe mlaji sana.

“Ugali kusema ukweli nakula gorogoro nne siku moja kama ni lunch time. Gorogoro nne za mahindi zisiagwe nipikiwe, nikule pamoja na sukuma besheni nne. Sidanganyi, hii mwili ni ya kukula,” Isaac alisema.

Baba huyo wa watoto watatu alibainisha kuwa mbali na kula sana, pia anakunywa sana ikilinganishwa na binadamu wa kawaida.

“Chai kusema ukweli nakunywa vikombe vikombe kumi na mbili. Mikate nakula nane. Kama supper nakula mchele na maharagwe, mchele katika kilo sita na maharagwe gorogoro mbili,” aliongeza.

Pia alidai kuwa kawaida huwa anakunywa lita thelathini za maji kwa siku.

Isaac aliibuka mitandaoni mapema mwezi huu, baada ya mwanamume mrefu mwenzake Bradley Marongo kupata umaarufu akidaiwa kuwa mwanamume mrefu zaidi nchini Kenya. Aliibuka akimpinga Bradley akidai kuwa ni mrefu kuliko yeye.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, mamake Isaac, Be Janet Nekesa aliweka wazi kwamba alikuwa na furaha kwa kujifungua mtoto huyo wake na kwamba alimlea vizuri bila matatizo mengi.

Alisema kuwa Isaac alikuwa mtoto mwenye afya nzuri na hakuwahi kuugua hadi alipokuwa na umri wa miaka kumi na tatu ambapo aliugua malaria kidogo.

“Nilimlea tu huku nyumbani Bungoma. Ukiangalia Isaac, ni Mungu tu alitaka aweze kusema jambo lisilo la kawaida. Amekuwa mtu mrefu, na mwili wak umekuwa mkubwae. Wenzangu walikuwa wakinitembelea wananiuliza nalisha nini mtoto?. Nilisema tu ni kazi ya Mungu,”  alisimulia katika mahojiano na Raipenda Evans.

Mama ya Isaac alisema anafurahishwa na ukuaji wa mwanawe akibainisha kwamba amekomaa, amepata mke, na hata amemzalia wajukuu watatu.

Pia alifichua kwamba alitatizika sana kupata mtoto katika miaka mitano ya kwanza katika ndoa yake  kabla ya Isaac kuzaliwa.

“Nilibarikiwa na Isaac kama mtoto wangu wa kwanza, nilifurahia tena nikapenda Mungu kwa sababu sio rahisi kutenda jambo kama hilo. Ilikuwa tu maajabu, kama muujiza wa Mungu kwa sababu labda Mungu alitaka kujionyesha yeye ni Bwana,” alisema

Aliendelea, “Kwa ndoa yangu nilipooleka, nilimaliza karibu miaka tano bila kupata mtoto. Nikawa wa kudharauliwa, nikawa wa kuchekelewa lakini nikamtegemea Mungu. Baada ya miaka tano, Mungu naye ni nani, nilibarikiwa nikaona nimepata mimba.”

Bi Janet alisema kuwa alijifungua mtoto wake nyumbani na baadaye akaenda naye kliniki kwa uchunguzi.

“Alipozaliwa alikuwa kilo tano, mpaka wenye nilikuwa nao kwa boma wakashangaa, ata mama mkwe alishangaa huu ni muujiza tu,” alisema.

View Comments