In Summary

•Fahyma alishangaa kama mpango wa mpenzi wake ni kuwasubiri wazeeke kama hivyo ili achukue hatua kama hiyo. 

•Haya yanajiri zaidi ya mwaka mmoja baada ya wazazi wenza hao walio na mtoto mmoja wa kiume pamoja kurudiana.

Image: INSTAGRAM// FAHYMA

Mpenzi na mzazi mwenza wa Rayvanny ,Fahyma almaarufu Fayvanny, anaonekana kuchoka kabisa kusubiri staa huyo wa bongo fleva amvishe pete ya uchumba kidoleni.

Siku ya Alhamisi, mama huyo wa mtoto mmoja wa kiume alichapisha video ya mwanamume mzee mwenye upara na ndevu zenye mvi akimchumbia mpenzi wake katika hafla ya kupendeza.

Katika sehemu ya maelezo ya video hiyo, Fahyma alishangaa kama mpango wa mpenzi wake ni kuwasubiri wazeeke kama hivyo ili achukue hatua kama hiyo. Alisema haelewi kabisa mipango ya mwimbaji huyo wa bongo fleva kuhusu mahusiano yao ya miaka mingi.

“@rayvanny unasubili tuzeeke kama ivi au? Maana sikuelewi ujue,” Fahyma aliandika.

Haya yanajiri zaidi ya mwaka mmoja baada ya wazazi wenza hao walio na mtoto mmoja wa kiume pamoja kurudiana, baada ya kutengana kwa zaidi ya miaka mitatu.

Mapema mwezi ulliopita, Rayvanny alimsherehekea mke huyo wake mrembo wakati akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Katika ujumbe mzuri aliomwandikia mpenziwe kwenye mtandao wa Instagram, bosi huyo wa lebo ya Next Level Music alitambua urembo wa mama huyo ya mwanawe na kumthamini kwa kumchagua yeye badala ya wanaume wengine wote.

Rayvanny alibainisha kuwa tayari walikuwa wamepitia changamoto nyingi katika uhusiano wao lakini akashukuru kuwa Fahyma ameendelea kusimama naye.

“Sura yako na uzuri ulionao ungeweza kwenda kwa yoyote ile ukanichagua mimi, Mengi tumepitia lakini bado upo upande wangu ❤️‍🔥,” Rayvanny aliandika.

Msanii huyo wa zamani wa WCB  aliambatanisha ujumbe wake na picha ya mkewe mrembo na kuendelea kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa.

“Wewe sio tu Mwanamke ila ni Mama !!! Mama Ake Chui @fahyvanny 🐆 NAKUPENDA SANA !!! Happy birthday maisha yangu!!! Enjoy Your Day,” aliandika.

Wakati akimjibu baba huyo wa mtoto wake, Fahyma pia alithibitisha kumpenda sana mwimbaji huyo na kuahidi kuendelea kumpenda.

“Nakupenda sana mume wangu na nitakupenda leo, kesho mpaka milele,” alijibu.

Fahyma ambaye pia anatambulika kama Fayvanny na mzazi mwenzake, Rayvanny wamekuwa wakionyesha mapenzi mazito baina yao tangu warudiane mapema mwaka jana baada ya awali kutengana takriban miaka mitatu iliyopita.

Mwezi Aprili mwaka jana, Rayvanny alidhihirisha mapenzi yake kwa mzazi huyo mwenzake kwa kuchorwa jina lake kwenye kifundo cha mkono wake.

"Fahyma...❤," ilisomeka tattoo mpya ya mwimbaji huyo.

View Comments