In Summary

•Bi Nyamu amejiunga katika kukashifu madai ya visa vya unyanyasaji wa kingono katika Kamba Festival mnamo Septemba 14.

•Seneta Mutinda alidai kukamatwa kwa washukiwa na akakashifu visa vya unyanyasaji wa wanawake.

Karen Nyamu wakati wa Kamba Festival.
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu amejiunga katika kukashifu madai ya visa vya unyanyasaji wa kingono wakati wa hafla ya hivi majuzi ya Kamba Festival katika uwanja wa Carnivore.

Bi Nyamu alikuwa mmoja wa waliohudhuria Tamasha la Kamba lililofanyika Septemba 14, na baadhi ya madai ya unyanyasaji wa kijinsia katika hafla hiyo yameibuka.

Siku ya Alhamisi, wanadada wawili walioandamana na seneta wa kuteuliwa Tabitha Mutinda waliandikisha ripoti katika Kituo cha Polisi cha Lang’ata, na kutaka kukamatwa kwa watuhumiwa wa uhalifu ambao walidai kuwa ni walinzi.

"Ilikuwa ya kusikitisha sana, yeye (mshukiwa) alikuwa akiwalenga wanawake ambao hawakuwa na watu wa kuwalinda," mmoja wa waathiriwa aliambia waandishi wa habari baada ya kuandikisha ripoti.

Mwathiriwa wa pili alilalamika kwamba unyanyasaji aliokumbana nao ulimuacha akiwa na kiwewe ilhali alitarajia usiku uliojaa furaha wakati akihudhuria hafla hiyo.

OCPD wa Langata Wanjiru Kimani alithibitisha kuwa wamepokea ripoti za unyanyasaji wa kingono na akabainisha kuwa uchunguzi kuhusu madai hayo umeanza.

"Baada ya kutoa ripoti hii alasiri ya leo, polisi wameanza uchunguzi wao," Bi Kimani alisema.

Seneta Mutinda alidai kukamatwa kwa washukiwa na akakashifu visa vya unyanyasaji wa wanawake.

Huku akikashifu kitendo hicho, seneta wa kuteuliwa Karen Nyamu alimshukuru mwenzake kwa kuwasaidia waathiriwa kuripoti na kutaja matukio hayo kuwa ya kusikitisha.

“Ripoti za unyanyasaji wa kijinsia katika Tamasha la Kamba ni za kuudhi na za kusikitisha. Ninalaani kwa maneno makali zaidi!” Nyamu alisema.

Waandalizi wa Tamasha la Kamba mapema wiki hii walikuwa wamekashifu visa vinavyodaiwa kuwa vya unyanyasaji wa kingono na kutoa pole kwa waathiriwa.

Walijitenga na madai hayo na kuthibitisha kuwa wanashirikiana na mamlaka katika uchunguzi huo.

View Comments