In Summary

•Akothee alizika wasiwasi kuhusu hali ya ndoa yake na kubainisha hajaachana na mumewe Denis Shweizer almaarufu Omosh.

•Akothee alibainisha kuwa ex wake Nelly Oaks bado kuwa maishani mwake haina athari yoyote mbaya katika ndoa yake

Akothee na mkewe Denis Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee ameweka wazi kuwa bango la ‘Niko Single Tena!' ambalo alichapisha siku ya Jumanne lilikuwa tangazo tu la wimbo wake mpya ‘Simu.’

Akiongea kwenye video siku ya Jumanne jioni, mama huyo wa watoto watano alizika wasiwasi kuhusu hali ya ndoa yake ya miezi mitatu na kubainisha kwamba hajaachana na mumewe Denis Shweizer almaarufu Omosh

Mwimbaji huyo alivifokea vyombo vya habari kwa kumpigia simu ili kufafanua kuhusu bango lake akibainisha kuwa ilikuwa wazi kuwa ni tangazo la wimbo.

“Huoni kwamba Niko Single ni wimbo! Unanipigia simu kuniuliza nimeachana na mume wangu kwa nini? Ni nini kingetufanya tuachane? Kwa sababu tu ya Nelly, sehemu ya familia yangu alikuja kwenye uzinduzi wa biashara ya binti yangu? Au ni kwa sababu nyote mmepoteza akili? Yaani nani anapanga bango la kusema ako single? Tumefikia kiwango hicho?" Akothee alifoka.

Aidha, alitangaza kuwa tayari ameachia kibao kali kwenye YouTube na kuwaomba mashabiki wake kuzamia kwenye mtandao huo na kukisikiliza.

Wakati huo huo, Akothee alibainisha kuwa meneja wake na ambaye ni mpenzi wake wa zamani, Nelly Oaks bado kuwa maishani mwake haina athari yoyote mbaya katika ndoa yake. Alisema mumewe Omosh yuko sawa na meneja huyo wake na hata yuko tayari kukutana naye.

“Mkae mkijua Nelly ni familia milele. Hao wenye wako kwa DM ya Omosh, mkae mkijua Nelly ni familia milele. Na hakuna mtu atamtoa hapo, Nelly sio ex. Hata Omosh anamjua, hata Omosh alisema akikuja Kenya watashiriki kinywaji pamoja," alisema.

Mwimbaji huyo aliwakosoa Wakenya ambao walidhani kwamba Nelly kuwa maishani mwake ni tatizo kwa ndoa yake akibainisha kuwa watajisikia vibaya wakati wakimwona akishiriki kinywaji na mumewe.

"Acheni upuuzi huo, ndivyo mnavyoniombea, mtu yeyote anayeandika kwamba Akothee ameachana na mumewe, ndivyo unavyoniombea," alisema.

Wikendi, Akothee alieleza kwa nini Nelly Oaks atakuwa karibu naye kila wakati licha ya kutengana kwao kimahusiano.

Alimtaja kama sehemu ya familia yake na akamshukuru kwa kusimamia chapa ya Akothee na kuwatunza watoto wake.

“Tunatoka mbali. Babu yake aliacha urithi katika jamii yangu. Unapomwona Nelly karibu nami, sijali unachotaka kufikiria.. Nelly asante kwa kuwa kila wakati kwa chapa ya Akothee na kwa kuwa kila wakati kwa watoto wangu. Anawatunza watoto wangu. Wanatoka pamoja, wanacheza densi. Wanangu wanampigia simu kila siku. Unapotuona, sisi ni familia," Akothee alisema wakati wa uzinduzi wa biashara ya bintiye Vesha Okello.

View Comments