In Summary

•Mwanamke huyo alisisitiza kuzungumza na Akothee akidai maisha yake yamo hatarini kwani kuna watu hatari wanaopanga njama dhidi yake.

•Nelly Oaks pia alimfichulia kwamba mwanamke huyo huyo pia aliwasiliana naye na kumwambia madai kama hayo.

Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwanamuziki na mfanyibiashara mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amefichua mwanamke ambaye alimtafuta kwa simu akiwa na nia ya kumlaghai.

Katika chapisho la Jumapili jioni, mama huyo wa watoto watano alionyesha screenshots za mazungumzo yake ya WhatsApp na mwanamke huyo aliyejitambulisha kama Rael Omedi.

Akothee alisema kuwa mlaghai huyo alisisitiza kuzungumza naye akidai kuwa maisha yake yamo hatarini kwani kuna watu hatari wanaopanga njama dhidi yake.

“Jamani, kuweni makini na Namba hii 0707***656. Alisisitiza kuzungumza nami ili kuokoa maisha yangu.Kisha akaendelea kusema alikuwa katika mkutano wa faragha na mwanasiasa mwanamke kutoka kaunti ya Migori ambaye alikuwa akinipangia mambo mabaya sana. Alisema kwamba anachumbiana na mmoja wa washikaji wa mwanamke huyo na hivyo ndivyo alivyoweza kuwa sehemu ya mkutano huo,” Akothee alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Kulingana na Akothee, mwanamke huyo aliyewasiliana naye alidai kuwa meneja wake, Nelly Oaks ni sehemu ya kundi linalopanga njama dhidi yake.

Kwa sababu ya imani yake kwa Nelly Oaks, mwimbaji huyo aliyezingirwa na drama sio haba hata hivyo alikuwa na imani sana kwamba mpenzi huyo wake wa zamani hangeweza kushiriki katika mipango mibaya dhidi yake.

"Alisema ilimsikitisha kwa sababu mtu wangu wa karibu sana, Meneja wangu Nellyoaks alikuwa sehemu ya mpango huo🤣🤣🤣🤣. Hapo ndipo nilipogundua, Ahhhhh sasa hapo umechoma , sio Nelly Oaks wangu, labda wako. Lakini sikumwambia. Kwa hiyo mwisho wa maongezi akasema ana rekodi na nimueleze ni kiasi gani naweza kulipia audio na kilichokuwa kinamuuma ni kwamba Nelly alikuwa sehemu ya mpango huo. Nilimwambia sihitaji sauti kwa vile sina uhusiano wowote na siasa, kisha akasema maisha yangu yako hatarini, kwa hivyo nikamwambia nitarejea kwake,” alisimulia.

Baada ya mazungumzo hayo, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 kisha alipiga hatua ya kuwasiliana na Nelly Oaks kuhusu madai hayo na kama alivyofikiria, meneja huyo wake alithibitisha kwamba hakuwa amehudhuria mkutano kama huo.

Nelly Oaks pia alimfichulia kwamba mwanamke huyo huyo pia aliwasiliana naye na kumwambia madai kama hayo.

View Comments