In Summary

•Okari alifichua kwamba hakuwahi kulipa mahari yoyote kabla ya kumuoa mke wake takriban miaka minne iliyopita.

•Alisema alipowatembelea wakwe zake akiandamana na babake na wajomba zake, hawakudai chochote kutoka kwao kama mahari.

Dennis Okari na mkewe Naomi Joy
Image: INSTAGRAM// DENNIS OKARI

Wikendi, mwanahabari wa uchunguzi Dennis Okari alifichua maelezo kuhusu mchakato wa kipekee wa ndoa yake na mkewe Naomi Joy.

Akizungumza wakati wa mkutano wa Daughters of Zion uliofanyika katika Kanisa la Jubilee Christian Church siku ya Jumamosi, mwanahabari huyo wa zamani wa NTV alifichua kwamba hakuwahi kulipa mahari yoyote kabla ya kumuoa mke wake takriban miaka minne iliyopita.

“Sikuwahi kutoa mahari, ukiingia kwenye ndoa unajifunza ni sawa na mapatano, mimi na mke wangu tulikaa nikamwambia ‘hizi ndizo pesa ninazo kwenye akaunti yangu, wajomba zako wakitaka kunitoza ng'ombe 10 na vitu vingine sina pesa ya aina hiyo. Nataka kukupa harusi, nikupeleke sehemu nzuri kwa fungate na nikutengenezee nyumba ila kwa sasa sina pesa ya aina hizo,” Okari alisema.

Okari alisema kuwa baada ya kumueleza mkewe kuhusu mpango wake alikwenda kwa mzazi wake na kuwaomba wasidai mahari kutoka kwake.

Alisema alipowatembelea wakwe zake akiandamana na babake na wajomba zake, hawakudai chochote kutoka kwao kama mahari.

"Ahadi niliyompa mke wangu ilikuwa, 'nitamfanyia mama yako kitu, na mwaka mmoja baadaye, nilimjengea nyamba mpya'," Okari alisema.

Mwanahabari huyo wa zamani wa NTV alibainisha kuwa mahari mara nyingi huwa na tatizo kwa wanaume wengi kwani wakati mwingine wakwe huwaagiza kutoa kiasi ambacho hawawezi kumudu.

Dennis Okari na Naomi Joy walifunga pingu za maisha katika hafla iliyohudhuliwa na wageni waalikwa pekee katika Kanisa la Ridgeways Baptist jijini Nairobi mnamo Februari 15, 2019. Hii ilikuwa takriban miaka mitatu baada ya ndoa ya Okari na mwanahabari mwenzake Betty Kyallo kuvunjika.

Wakati akizungumza siku ya Jumamosi, mwanahabari huyo wa zamani wa NTV alifunguka kuhusu mawazo ya kutaka kujidhuru ambayo yalimsumbua kufuatia talaka yake.  Okari alikiri kwamba talaka yake na mama huyo wa bintiye ambayo ilikuja miezi michache tu baada ya harusi yao ya kifahari ilimuathiri sana.

Alifichua kwamba wakati fulani alifikiria kusababisha ajali na gari lake ili kupoteza fahamu na kusahau masaibu yake.

"Nilikuwa nikiendesha gari kwenye Mombasa Road na nilifikiria kusababisha ajali na gari langu ili niende kwenye koma, na wakati nikiamka, yote hayo yawe yamepita. Nilitafuta jiwe lililokuwa barabarani lakini sikuweza kuliona usiku huo,” Okari alisimulia.

Alisema, "Kamwe hufungi ndoa ili kutaliki."

Okari na Betty Kyallo walichumbiana kwa takriban miaka minne kabla ya kufunga ndoa katika harusi ya kupendeza mnamo Oktoba 2, 2015 katika bustani la Marula Manor, mtaa wa Karen, jijini Nairobi. Kwa bahati mbaya, wanahabari hao wawili waliamua kutengana na kwenda njia tofauti takriban miezi sita tu baadaye.

View Comments