In Summary

• Zulu alihoji kwamba nyinyi wote kuwa na watoto kutoka mahusiano yenu ya awali haina maana kwamba mnaendana kimaadili.

Mwanasaikolojia Benjamin Zulu
Image: Facebook

Mwanasaikolojia Benjamin Zulu anahoji kwamba si vibaya kuoana na mchumba ambaye tayari ana mtoto kwani si kila mwenye mtoto alimpata kimakosa.

Kulingana na Zulu, kigezo pekee cha kuangalia na kutathmini mtu aliye na mtoto kabla ya kumuoa ni kuchunguza iwapo baada ya kupata mtoto, mtu huyo alijifunza kutokana na hali hiyo na pengine kubadilika.

“Mtu aliuliza nini cha kuzingatia wakati wa kuoa mtu aliye na mtoto na nikasema angalia tu ikiwa walikua na uzoefu. Iwapo walijifunza na kubadili tabia zao. Sio kila mtu alipata mtoto kwa makosa. Kwa wengi ilikuwa tu matunda ya mtindo wao wa maisha na mtazamo wao kuhusu ngono na hawajabadilika,” alihoji Zulu.

Zulu anashauri kwamab kimsingi, mtu unafaa kuoa mchumba ambaye mnaendana kimaadili na kimitindo pia na kusema kwamba kuwa na mtoto na yeye kuwa na mtoto si kigezo tosha cha kusema kwamba mnaendana kwa sababu kila mtu alibadilika kivyake baada ya kupata mtot; wengine wakabadilika vizuri na wengine vibaya.

“Na kwa sababu una mtoto na wao pia wana mtoto haimaanishi kuwa unashiriki maadili. Baadhi ya watu walibadilika na kuwa bora baada ya tukio hilo na unaweza kujua kwa sababu hawawezi tena kufanya ngono kabla ya ndoa. Wengine walijifunza tu 'kuwa makini zaidi' ambayo ina maana ya kuepuka mimba au kupunguza mara kwa mara ya tendo lakini bado ni mtu yule yule,” mwanasaikolojia Zulu anashauri zaidi.

Pia Zulu alizungumzia suala la kuzingatia vigezo vingi kama hivyo ili kuepuka drama zinazotokana na uzazi wa kushirikiana kulea mtoto huku wazazi wote wakiwa hawaishi tena pamoja, almaarufu ‘co-parenting’ kwa kimombo.

Zulu alisema kama mchumba wako ana mtoto na hajalainisha mambo na mzazi mwenziwe basi huyo bado ana misukosuko na hawezi kuwa na amani ya akili kuwa katika mahusiano mapya.

“Ikiwa hawajafanya kazi ya kurejesha utulivu na amani maishani mwao, hawako tayari kwa muungano wenye amani. Hata kama mzazi mwingine ana machafuko lazima uone jinsi mtu huyu amerejesha mipaka na kuondoka mahali hapo kama mtu. Ikiwa hawakukua na kubadilika kimakusudi, bado wako katika njia ile ile na hata ukiwaoa wataendelea kufanya usaliti,” Benjamin Zulu alihoji.

View Comments