In Summary

•Guardian Angel alitaja uhusiano wake na mama huyo wa watoto watatu wakubwa mwenye umri wa miaka 53 kuwa muunganisho sahihi.

•Guardian alifichua kwamba ameweza kukua katika nyanja nyingi za maisha tangu alipojuana na mwenzi huyo wake wa maisha.

Image: INSTAGRAM// GUARDIAN ANGEL

Mwimbaji wa nyimbo za injili Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel amebainisha kuwa amepata mafanikio mengi katika miaka minne ambayo amekuwa kwenye mahusiano mke wake  Esther Musila.

Akizungumza kwenye mahojiano ya YouTube na Willy M. Tuva , Guardian Angel alitaja uhusiano wake na mama huyo wa watoto watatu wakubwa mwenye umri wa miaka 53 kuwa muunganisho sahihi.

“Yamebadilisha maisha yangu, ukimsikiliza akiongea (Bi Musila) atasema jinsi mahusiano yetu yamebadilisha maisha yake,” alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 33 alidokeza kuwa athari chanya ya mahusiano yao ndilo jambo muhimu zaidi bila kujali maneno hasi kutoka ya wakosoaji .

Aidha, alifichua kwamba ameweza kukua katika nyanja nyingi za maisha tangu alipojuana na mwenzi huyo wake wa maisha.

“Nimeweza kuwa na ufanisi, nimeweza kukua, sio tu kimwili, lakini nimeweza kukua hata kiuchumi. Hata vitu kama hii ukulima yangu, na sifanyi ukulima kwa shamba ya watu, nafanya kwangu. Hiyo yote imeweza kufanyika kwa sababu ya muungano ambao niko nao na mke wangu," alisema Guardian Angel.

Mwanamuziki huyo alikashifu wote wanaopinga ndoa yake akisema kuwa wao ni watu wenye wivu na wapuuzi. Kufuatia hilo, aliwataka kuzingatia kuboresha maisha yao na kuacha kujiingiza katika biashara za watu wengine.

Guardian hata hivyo alikiri kuwa matusi mengi ambayo huelekezwa kwa mkewe kwa kawaida hufanya ahisi vibaya.

"Naskia vibaya sana. Kwa kweli najisikia kuchukizwa sana na kuguswa sana kwa sababu huyu ni mtu ninayempenda sana. Sisi sote tunaweza kuona hilo," alisema.

Alisema kwamba ndoa yake imekuwa mzuri huku akibainisha kuwa kuna wanaume wengi ambao wameoa wanawake wadogo kiumri lakini wanaishia kutengana.

View Comments