In Summary

•Vera  alisema anaona kila kitu kuhusu hali yake mpya kikiwa kizuri na anafurahishwa sana na majukumu ya mama.

•Vera alisema angependa kupata watoto wawili wa kiume na mwingine mmoja wa kike ili kuwe na usawa katika familia yake.

Image: INSTAGRAM// VERA SIDIKA

Mwanasoshalaiti na mtumbuizaji mashuhuri nchini Kenya Vera Sidika ameonekana kuendelea kufurahia hali ya kuwa mama miezi takriban miezi mitatu baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza, Asia Brown.

Alipokuwa anashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu, Vera  alisema anaona kila kitu kuhusu hali yake mpya kikiwa kizuri na anafurahishwa sana na majukumu ya mama.

Mpenzi huyo wa mwanamuziki Brown Mauzo ameweka wazi kwamba inapokuja kwa bintiye na watoto atakaopata baadae, siku zote ataweka hadhi yake ya mtu mashuhuri kando na kutekeleza majukumu ya mama ifaavyo.

"Ikikuja kwa Asia ama watoto nitakaopata baadae, hakuna umashuhuri. Mimi ni mama, mama mzuri kusema kweli... Hakuna hasara kwa kupata mtoto, sio shughuli nyingi. Kila kitu ni kizuri, najizungumzia lakini. Nabadilisha nepi ya Asia mara kwa mara na nacheka na kutabasamu naye. Kila kitu nikizuri kweli. Hata mambo ambayo huenda yakakera mwingine, kwangu ni mazuri" Vera alisema.

Mwanasoshalaiti huyo pia alidhihirisha kuwa bado hajafunga tumbo lake la uzazi huku akifichua anapanga kupata angalau watoto wengine watatu.

Vera alisema angependa kupata watoto wawili wa kiume na mwingine mmoja wa kike ili kuwe na usawa katika familia yake. Alisema aliumwa sana kukua bila dada na hangependa bintiye apitie masaibu kama yale.

"Kusema kweli nataka watoto wanne. Natumai kupata wavulana wawili na wasichana wawili. Hivyo Asia atakuwa na dada na kaka wawili. Mvulana ambaye nitapata atakuwa na kaka na dada wawili. Huo ni usawa mzuri. Kwetu tulikuwa watatu na nilikuwa msichana pekee. Iliniuma sana kukua bila dada." Alisema Vera.

Mama huyo wa mtoto mmoja pia alifichua kuwa mumewe anafurahia majukumu ya baba na ana uhusiano mzuri sana na binti yao.

View Comments