In Summary

•Staa huyo wa Mugithi alishiriki picha nzuri ya Tiana akiwa ameshika mdoli na kuisindikiza na wimbo wa ‘My Wish’ wa Rascal Flatts.

•Samidoh alikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya binti huyo mdogo.

Samidoh alikuwa miongoni mwa waliohudhuria karamu ya siku ya kuzaliwa ya bintiye Karen Nyamu.
Image: INSTAGRAM// KAREN NYAMU

Mzaliwa wa kwanza wa Seneta wa Kuteuliwa Karen Nyamu, Tiana aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa jana, Agosti 24.

Watu wa karibu akiwemo mwanasiasa huyo na mzazi mwenzake DJ Saint Kevin walijitokeza kumsherehekea hadharani msichana huyo wakati akitimiza umri wa miaka 9.

Mpenzi wa seneta Nyamu na ambaye ni baba wa watoto wake wengine wawili, mwimbaji Samuel Muchoki almaarufu Samidoh pia hawakuachwa nyuma. Katika ukurasa wake, staa huyo wa Mugithi alishiriki picha nzuri ya Tiana akiwa ameshika mdoli na kuisindikiza na wimbo wa ‘My Wish’ wa Rascal Flatts.

Chini ya video hiyo, Samidoh aliandika ujumbe mzuri kwa msichana huyo mdogo ambapo alimtakia heri anapopiga hatua mwaka mmoja zaidi.

"Msichana mdogo wa kushangaza, endelea kuangaza, mwaka wako ujazwe na nyakati za kusisimua na tabasamu zisizo na mwisho. Kheri ya siku ya kuzaliwa,” Samidoh aliandika.

Staa huyo wa Mugithi pia alikuwa miongoni mwa wageni waliohudhuria karamu ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya binti huyo mdogo kama ilivyoonyeshwa kwenye picha zilizoshirikiwa na seneta Karen Nyamu.

“Cha muhimu ni birthday girl askie fiti na marafiki na familia,” Karen Nyamu aliandika chini ya picha za siku hiyo ya kuzaliwa alizochapisha kwenye Instagram.

Katika kumsherehekea binti yake wa kwanza, seneta Nyamu alitimiza matakwa yake ya siku ya kuzaliwa ya kupanda treni ya SGR.

Kulingana naye, malkia huyo mdogo aliomba kuabiri SGR na seneta huyo alibainisha kuwa pia yeye alifurahia sana safari ya treni.

“Kwa hiyo juzi nilipanda SGR kwa mara ya kwanza kabisa, shukrani kwake (Tiana). Ilikuwa ombi lake la siku ya kuzaliwa. Niliipenda,” Karen Nyamu aliandika chini ya video yake na bintiye huyo ndani ya treni ya SGR aliyoichapisha kwenye Instagram.

Seneta huyo wa UDA aliendelea kukiri upendo wake mkubwa kwa mzaliwa huyo wake wa kwanza na kukiri jinsi anavyojivunia kuwa mzazi wake.

"Siku ya kuzaliwa yenye furaha kwa msichana mzuri zaidi, mwenye talanta zaidi, mwenye furaha zaidi na mwenye upendo zaidi. Najisikia heri kuwa mama yako mtoto,” alisema.

Baba ya msichana huyo mdogo, mcheza santuri DJ Saint Kevin pia alimwandikia ujumbe mtamu wa kuadhimisha siku yake maalum.

Katika ukurasa wake wa Instagram, mburudishaji huyo alishiriki picha yake nzuri na Tiana na kwenye sehemu ya maelezo, alieleza upendo wake mkubwa kwake.

Katika ujumbe wake, Saint aliizungumzia jinsi binti yake anavyosisimua maisha yake na ya watu wengine karibu naye.

"Heri ya kuzaliwa kwa binti yangu wa kifalme ambaye hunifanya nione maisha katika rangi kamili! Unaongeza furaha kwa kila mtu unayekutana naye na leo tunasherehekea uzuri wa kufurahisha ulio nao. Nakupenda mtoto wangu,” DJ Saint Kevin aliandika.

DJ Saint ndiye baba wa mtoto wa kwanza wa Karen Nyamu. Wawili hao walichumbiana kwa kipindi kabla ya kwenda njia tofauti.

View Comments